Mwalusako: TFF siyo sehemu ya majaribio chagueni viongozi wanaojua matatizo ya mpira

Muktasari:

Mwalasako aliyewahi kuwa Katibu mkuu wa klabu ya Yanga alisema ifike mahali wapiga kura na wagombea waheshimu shirikisho hilo kwa kuchagua viongozi ambao wataleta maendeleo ya soka na kuacha tabia ya kubebana kutokana na undugu ama urafiki.

Dar es Salaam. Mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Lawrence Mwalusako amewaambiwa wagombea na wapiga kura katika uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuwa shirikisho hilo siyo sehemu ya majaribio na anayeingia hapo lazima afuate misingi ya soka.

Mwalasako aliyewahi kuwa Katibu mkuu wa klabu ya Yanga alisema ifike mahali wapiga kura na wagombea waheshimu shirikisho hilo kwa kuchagua viongozi ambao wataleta maendeleo ya soka na kuacha tabia ya kubebana kutokana na undugu ama urafiki.

Mwalusako alisema kuwa; "Tunahitaji ligi bora na Taifa Stars yenye ushindani mkubwa ambayo inaweza kufika mbali katika mashindano mbalimbali, hicho ni kipimo cha maendeleo ya soka letu na si vinginevyo.

Pia,  tuache tabia ya kubebana kuingia madarakani kwanza inatakiwa damu changa na hasa waliowahi kucheza mpira kwani wanajua zaidi.

"Kuna viongozi ambao hawajacheza mpira, lakini wanaoongoza vizuri soka ila wanapaswa kushirikiana na watu waliocheza mpira ambao nao wawe ni miongoni mwa wachezaji, Tenga alifanikiwa kwa kiasi fulani japokuwa hakuwa na timu imara ya kumsaidia," alisema Mwalusako.

Kiongozi huyo alisema kuwa anaamini kila kiongozi anayeingia madarakani anakuwa na ilani yake hivyo wanapaswa kutimiza ilani na kwamba kiongozi ambaye hajatimiza ilani yake hapaswi kuchaguliwa.

"Ilani ndiyo kila kitu, kama kiongozi hajatimiza ilani yake kwanini umchague tena, huyo anakuwa hapaswi wala hafai kuendelea kuongoza," alisema Mwalusako.