Chipukizi Masanja apiga bao sita, Mwanza ikiua Kagera 10-1 katika michezo ya Umitashumta

Muktasari:

Mchezo huo ulianza kwa timu zote kuonekana kuwa na nguvu sawa, lakini ghafla mambo yalibadilika kwa Kagera kuanza kupokea kipigo bila majibu.

Mwanza. Hii sasa sifa. Mshambuliaji wa timu ya soka ya Wavulana Mkoa wa Mwanza, Joseph Masanja alifunga mabao sita peke yake katika ushindi wa mabao 10-1 dhidi ya Mkoa wa Kagera katika michezo ya Umitashumta inayoendelea jijini Mwanza.

Mchezo huo ulianza kwa timu zote kuonekana kuwa na nguvu sawa, lakini ghafla mambo yalibadilika kwa Kagera kuanza kupokea kipigo bila majibu.

Mwanza ilipata bao kwanza dakika ya 18 kupitia kwa Joseph Masanja, ambaye alifunga mengine  matatu katika dakika ya 23, 29 na 33 kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili Kagera iliendelea kupoteana na kuwaruhusu wapinzani wao kuutawala mchezo na dakika ya 67, Masanja alifunga bao lake bao la tano na dakika ya 77, Edmund Geofrey aliongeza bao la sita.

Alphonce Mabula alifunga bao la saba, Masanja akaongeza la nane likiwa ni bao lake la sita dakika ya 81, kabla ya Cosmas Lucas kuhitimisha kalamu hiyo kwa kufunga bao la tisa na kumi.

Bao pekee la Kagera lilifungwa na Juma Aman kwa mkwaju w penalti dakika ya 86 baada ya mabeki wa Mwanza kuunawa mpira katika eneo la hatari.

Mechi nyingine, netiboli, Dodoma ikaichapa Kagera kwa magoli 21-6, huku Mara ikiilaza Simiyu magoli 24-11.

Mpira wa mikono wasichana, Simiyu ilipoteza mabao 8-7 dhidi ya Katavi na Kigoma ikaidunda

Ruvuma mabao 3-0.

Kwa wavulana Rukwa iliidundwa mabao 6-5 dhidi ya Mara na Songwe ikachapa Dodoma mabao 14-9.