Dar, Kigoma, Mara zapata kashfa ya kuchezesha wachezaji vijeba michezo ya Umitashumta

Muktasari:

Jumla ya Mikoa 26 ya Tanzania Bara inashiriki mashindano hayo yenye lengo la kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana kupitia Shule za msingi baada ya ile ya Sekondari (Umisseta) kumalizika.

Mwanza. Mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Tanga na Mara zimetajwa kuwa vinara wa kuwachezesha wanafunzi waliozidi umri ‘vijeba’ kwenye mashindano yaUmitashumta yanayoendelea jijini hapa.

Jumla ya Mikoa 26 ya Tanzania Bara inashiriki mashindano hayo yenye lengo la kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana kupitia Shule za msingi baada ya ile ya Sekondari (Umisseta) kumalizika.

Wanafunzi hao wamebainika baada ya kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya Walimu na Makocha kuilalamikia baadhi ya Mikoa kuwatumia wanafunzi hawana vigezo katika mashindano hayo.

Mwenyekiti wa Mashindano hayo kitaifa, Jeshi Lupembe alisema kuwa baada ya kupata malalamiko hayo,kamati iliunda tume maalumu iliyoshirikisha wataalamu wa soka kuchunguza wachezaji wasio na sifa.

Alisema kuwa katika uchunguzi walioufanya tayari wanafunzi saba kutoka mikoa mbalimbali walibainika kutokuwa na sifa na maamuzi ya kamati iliweza kuwasimamisha wachezaji hao kutoshiriki michezo yoyote.

“Baada ya malalamiko hayo,sisi kamati tuliunda tume maalumu ya kuchunguza wanafunzi hao na tayari tumewanasa wachezaji saba na kwa utaratibu tumewasimamisha kutocheza michezo yoyote,”alisema Lupembe.