Mshambuliaji Yanga amaliza ukame wa mabao

Muktasari:

Tangu kuanza kwa msimu huu Martin amefunga kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu

Dar es Salaam. Mabao mawili aliyofunga mshambuliaji Emmanuel Martin amesema yamemtoa kifungoni na kumpa amani ya moyo.

Martin alifunga mabao hayo wakati Yanga ikishinda 5-0 dhidi  Mbeya City, Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana Jumapili.

Martin hakusita kueleza ukweli namna alivyokuwa anajisikia vibaya kutofunga bao hata moja katika mechi tisa na kufanikiwa kufunga mechi ya 10, kwamba alikuwa anajiona kama mchango wake hauonekani.

"Asikuambie mtu Yanga ni klabu inayotetea ubingwa, kama mshambuliaji nilikuwa naumia sana, nikitoka kapa bila kufunga, hilo lilikuwa linavuruga hadi akili yangu."

"City imenifungulia njia ya kujiamini zaidi, kabla ya mzunguko wa pili naweza nikawa na mabadiliko ya hali ya juu katika nafasi yangu ya ufungaji,"alisema

Alitaja kilichoongezeka baada ya kufunga mabao hayo kwamba ni kujiamini na kuona anaweza akasogelea nyavu za wapinzani kwa mafanikio.

Kwa upande wa winga wa zamani wa timu hiyo, Ally Yusuph Tigana, alisema kuwafunga City, mabao 5-0 ni kama kimepunguza nguvu ya Simba.

"Yanga wakishinda kwa staili hiyo katika mechi mbili au tatu zijazo basi Simba, watakuwa hawana jipya, lasivyo wapambane sana kuhakikisha wanaongeza umakini kwenye umaliziaji,"alisema Tigana.