Mbinu za Majimaji zaipoteza Mbao

Muktasari:

Timu hiyo ya mjini Songea baada ya kuanza vibaya ligi sasa imerudi katika mstari na kutumia vizuri uwanja wa nyumbani

Mwanza. Kocha msaidizi wa Majimaji FC, Habib Kondo amewapongeza wachezaji wake kwa kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbao FC katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.

Katika mchezo huo mabao ya Majimaji FC yalifungwa na Japhary Mohamed katika dakika ya 45 na Marcel Boneventure aliyefunga kwa mkwaju wa penalti katika dakikaya 87.

Kondo alisema timu yake ilitawala mchezo huo na kutengeneza nafasi nyingi  katika vipindi vyote.

“Kiukweli tulistahili ushindi kwa kuwa vijana wangu walitengeneza nafasi nyingi  kuliko katika michezo yetu yote tuliowahi kucheza msimu huu,” alisema Kondo.

Habib alisema anawaomba mashabiki na wadau wa soka wa mkoani Ruvuma waendelee kuishangilia timu yao katika michezo yao iliyobakia.

Kocha mkuu wa Mbao FC, Etienne Ndairagije alisema timu yao ilizidiwa na wapinzani wao katika kumiliki mipira ya juu jambo lililochangia kushindwa kwao.

“Wapinzani wetu waliibua mbinu iliyotizi, lakini ni matumani yangu, tumejifunza kwa makosa haya,” alisema Mrundi huyo.

Ndairagije aliipongeza Majimaji kwa ushindi huo na alisema nguvu zote wanaelekeza katika mchezo wao dhidi ya Mwadui FC mechi itakayochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.