Yanga SC anzeni maandalizi mapema, hakuna kurudi nyuma

Muktasari:

  • Kundi hilo lina timu mbili za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Rayon Sport ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya pamoja na USM Alger ya Algeria, ambapo zote zitakuwa na kibarua cha kusaka uongozi wa kundi hilo ili kusonga mbele.

RATIBA ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika imeshatangazwa na mabingwa watetezi na wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye michuano ya klabu Afrika, Yanga imepangwa Kundi D.

Kundi hilo lina timu mbili za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Rayon Sport ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya pamoja na USM Alger ya Algeria, ambapo zote zitakuwa na kibarua cha kusaka uongozi wa kundi hilo ili kusonga mbele.

Yanga imetinga hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya kuiondosha Welaytta Dicha ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 2-1, na kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Dar es Salaam, Yanga ilishinda kwa mabao 2-0 na kwenda kupoteza kwa bao 1-0 kule Hawassa hivyo, kusonga mbele.

Mwanaspoti haliachi kuipongeza Yanga kwa kutinga hatua hiyo ya makundi, lakini kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Yanga ndio imeingia rasmi kwenye ushindani hivyo, haipaswi kujisahau kabisa.

Hatua ya makundi ni ngumu na kila timu imejipanga kuhakikisha inapata matokeo mazuri na kutinga hatua ya robo fainali ambako, kuna mamilioni ya fedha hutolewa kwa timu zilizofanya vizuri.

Kwanza kwa kuingia tu kwenye hatua ya makundi, Yanga itavuna zaidi ya Sh600 milioni, lakini timu itakayomaliza ya kwanza kwenye kundi itavuna.

Ni fedha hizo ndio zinazipa timu washiriki mzuka wa kupambana ili kufanya vizuri hivyo, Yanga wanapaswa kulitambua hilo na kuanza kujipanga mapema ili kufanya kweli.

Mwanaspoti limeona ni vyema kuwakumbusha Yanga kutokana na baadhi ya viongozi na wanachama kutamba kwamba, wamepangiwa kundi mchekea hivyo wana uhakika wa kusonga mbele kwenda hatua ya robo fainali.

Uwepo wa timu mbili za Afrika Mashariki ni kama umeanza kuwafanya watu wa Yanga kujiona kama wanaweza kupata matokeo mazuri kwa sababu tu ya kujuana kimbinu ama kwa kuangalia ligi zilizopo kwenye nchi hizo.

Hili linaweza kuwa tatizo kubwa na linaweza kuigharimu Yanga kwani, hatua waliyofikia kamwe hawatakiwi kudharau wapinzani wao hata kidogo. Ifahamike kuwa kila timu iliyotinga hatua ya makundi ina uwezo mkubwa na mipango ya maana na ndio sababu imeweza kusonga mbele huku zile ambazo hazina bahati ama mipango mibovu zimebaki nje ya michuano.

Kwa kuangalia tu wapinzani wa Yanga kwenye kundi hilo la D, wote wana historia kubwa kwenye soka na zimevuna mafanikio mengi hivyo, Wawakilishi wetu hao wanapaswa kujipanga kwelikweli.

Gor Mahia ni klabu kongwe kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ilianzishwa Februari 17,1968 ikijulikana kama Luo Union huku chimbuko lake likiwa miaka ya 1920.

Gor maarufu kama Kogalo ndio timu yenye rekodi tamu kwenye soka la Kenya na ndio mabingwa watetezi. Imebeba taji hilo 16 na msimu huu ndio vinara ikifukuzia rekodi ya kutetea taji lake hilo.

Pia, ina rekodi ya kuichapa Yanga kwenye michuano ya Kagame Cup hivyo, Yanga kamwe haipaswi kubweteka kwa kuamini wanaweza kutoka salama. Vivyo hivyo kwa Rayon Sport na USM Alger ambao rekodi zao sio za kitoto hata kidogo.

Lakini, pamoja na rekodi hizo za wapinzani wake kwenye kundi hilo, Mwanaspoti linatambua kuwa kama Yanga wataanza maandalizi mapema basi kila kitu kitakuwa rahisi na Tanzania inaweza kuandika historia mpya kwenye michuano hiyo.

Jambo la msingi ambalo Yanga inatakiwa kulifanya ni kuanza maandalizi mapema kwa kusajili wachezaji wenye viwango vya kupambana kimataifa ili kuwasaidia kufika mbali.

Tunatambua kuwa kwa sasa Yanga wapo kwenye vita kubwa ya kutetea ubingwa wao ambao, mahasimu wao Simba wako hatua chache kuufikia, lakini ni vyema hili la miachuano ya CAF likaenda pamoja. Yanga ihakikishe inawaanda wachezaji wake kisaikolojia na kuwapa mbinu mpya za kukabiliana na wachezaji wenye viwango vya juu walioko kwenye timu zingine. Tunasema hivyo kwa sababu, Yanga hii ambayo jana imetoa sare na Mbeya City imekuwa ikiundwa na kikosi cha kawaida kutokana na mastaa wake wakubwa kuwa majeruhi.

Pia, haina kocha mkuu kwa sasa baada ya George Lwandamina, kutimkia zake kwao kutokana na mambo kutokaa sawa klabuni hapo kwa sasa. Changamoto hizi ndani ya Yanga ni muhimu zikapatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuiwezesha Yanga kuwa na ushiriki wenye tija na kufika mbali zaidi.