Wenger adai Spurs itamuuza Harry Kane

Monday May 14 2018

 

ARSENE Wenger amesema Tottenham Hotspur wanakabiliwa na wakati mgumu na huenda wakaishia tu kwenye kumpiga bei straika wao matata, Harry Kane kwenye dirisha lijalo la usajili.

Wenger alisema kutokana na kukabiliwa na gharama za kujenga uwanja, jambo hilo linaweza kuwafanya Spurs kulazimika kuuza wachezaji wake nyota akiwamo Kane ili kupata pesa za kuongezea kwenye mipango yao.

Kwa sasa Spurs, wanafanya marekebisho ya uwanja wao wa White Hart Lane, ambao unaripotiwa kuwagharimu karibu Pauni 800 milioni. Wenger amesema hilo baada ya kujiweka yeye mwenyewe kuwa mfano kwamba wakati wanafanya ujenzi wa Uwanja wa Emirates, alilazimika kuwapiga bei wachezaji wake nyota ili kuipunguzia timu mzigo na jambo hilo linaweza kuigharimu Spurs. Wenger jana Jumapili alitarajia kuiongoza Arsenal katika mchezo wake wa mwisho akiwa kocha wa timu hiyo walipomenyana na Huddersfield ugenini.