Wako wapi makocha waliopita Simba, Yanga?-1

Muktasari:

  • Kuodoka kwa aliyekuwa Kocha wa Yanga, George Lwandamina, kumeifanya klabu hiyo kufikisha jumla ya makocha 20 ambao wamepita kuifundisha timu hiyo kwa kipindi cha miaka 18 iliyopita..

ONDOKA ingia za makocha ndani ya klabu za Simba na Yanga imekuwa kama tamthiliya ya Isidingo vile ambayo haijulikani lini itamalizika.

Kuodoka kwa aliyekuwa Kocha wa Yanga, George Lwandamina, kumeifanya klabu hiyo kufikisha jumla ya makocha 20 ambao wamepita kuifundisha timu hiyo kwa kipindi cha miaka 18 iliyopita..

Watani zao Simba nao hawana tofauti kwa kuwa ndani ya miaka hiyo, 18 wamepita makocha mara 18, kimahesabu timu hizo zimekuwa na wastani wa kubadili makocha kila mwaka tangu, 2000 mpaka sasa.

Wakongwe hao wa soka la Tanzania kwa pamoja wamebadili makocha mara 36 kwa miaka 18. Umewahi kujiuliza makocha hawa wako wapi na wanafanya nini? Haya jisomee mwenyewe.

RAOUL SHUNGU- YANGA

Kocha Mkongomani Raoul Shungu (60), alitimuliwa Yanga mwaka 2000 na alipata majukumu ya kuinoa Timu ya Taifa ya Shelisheli na baadaye akaibukia Rayon Sport ambapo alipata mafanikio ya kutwaa mataji matano.

Shungu alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Rwanda mara nne na mara moja Kombe la Ligi. Baadaye 2008 alipata majukumu mengine ya kuifundisha Timu ya Taifa ya Rwanda, kisha 2012 akajiunga na St. Eloi Lupopo ya nyumbani kwao. Kwa sasa hana timu.

PATRICK PHIRI- SIMBA

Phiri (61) ambaye ameifundisha Simba kwa awamu tatu tofauti, alipotimuliwa mwaka 2005 kwa awamu ya kwanza, alipata kibarua cha kuinoa Timu ya Taifa ya Zambia na kuipa Kombe la Cosafa, 2006.

Simba ni kama ilistuka na kumrejesha, 2008 ambapo ilikaa naye hadi 2011 na kuamua kumtimua tena. Baada ya kutimuliwa Phiri alirejea kwao, Zambia na kuifundisha, NAPSA Stars kabla ya kutimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa msaidizi wake, Peter Kaumba.

Agosti 2014, Simba ilifanya uamuzi wa kumrejesha Phiri kwa awamu ya tatu, hata hivyo Novemba ndani ya mwaka huo akatimuliwa na kutokomea.

MILUTIN SREDOJEVIC - YANGA

Sredojevic ‘Micho’ alitimuliwa Yanga 2007 baada ya kushindwa kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa. Kibarua chake kilivyoota nyasi fasta Saint-George SA ya Ethiopia ilimrejesha kundini. Micho kabla ya kuondoka St. George aliipa vikombe viwili vya Ligi Kuu na Ngao ya Hisani mara moja.

Alivyorejea kwa mara nyingine nchini humo akitokea Yanga, Micho aliipa tena klabu hiyo Ngao ya Hisani mwaka 2009 na baada ya hapo akashinda tena mataji mengine mawili ya Ligi Kuu.

Micho hakuishia hapo, mafanikio yake yaliendelea hata alipojiunga na Al-Hilal Omdurman ya Sudan ambayo aliifundisha kwa msimu mmoja na kuipa Kombe la Ligi Kuu na Kombe la ligi ‘FA’ nchini humo.

Unaweza kusema ni kama Yanga ilikuwa na papara kwa kumtimua Mserbia huyo kwani alipata pia ulaji wa kuinoa timu ya Taifa ya Rwanda ambapo kwenye Kombe la Chelenji ilishika nafasi ya pili mwaka 2011 na 2015 akaipa ubingwa wa mashindano hayo, Uganda.

Mchawi huyo wa soka la Afrika Mashariki, Micho kwa sasa ni Kocha wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini ambayo alikuwa akiifundisha kabla ya kutua Yanga.

DYLAN KERR- SIMBA

Kocha Kerr alifungashiwa virago vyake Simba mwaka 2016 na kurejea kwao Uingereza. Baadaye kocha huyo aliibukia Kenya kwenye klabu ya Gor Mahia ambayo ameipa ubingwa msimu uliopita wa Ligi Kuu.

Kerr anapambana msimu huu na Gor Mahia yake kutetea taji la ligi hiyo huku wakianza na kasi ya aina yake kwa kuwa nafasi ya pili ya msimo wa ligi huyo huku wakiwa wamecheza michezo minane.

Pamoja na kuwa na michezo mitatu mkononi, Gor imeachwa pointi moja tu na Mathare United yenye pointi 23 kileleni.

DUSAN KONDIC-YANGA

Mara baada ya kutimuliwa Yanga, Mserbia Kondic alipata mkataba wa miaka miwili ya kuinoa, Saint George S.C. ya Ethiopia na alivyojiunga nayo akatwaa ubingwa wa ligi hiyo, mwaka 2012, kwa sasa amekuwa kimya kocha huyo.

WANACHOSEMA WADAU

Nyota wa zamani ya Yanga, Sekilojo Chambua amesema timuatimua ya makocha kwa Simba na Yanga ni kutokana na presha zinazochochewa na mafanikio ya upande wa pili.

“Utulivu ndani ya klabu za Simba na huwa mdogo kwa namna yoyote ile hata akija kocha wa kiwango gani kama atafanya vibaya kwenye msimu wake wa kwanza, atatimuliwa bila kujali hadhi yake,” anasema.

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa anasema pengine mafanikio ya klabu hizo kwenye mashindano ya kimataifa.

Fuatilia simulizi hii katika toleo la kesho.