#WC2018: Sababu tatu Croatia kubeba Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Croatia maarufu kama ‘Watoto wa Mama’, walitinga hatua hii ikiwa kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa lao, baada ya kuwazima wajukuu wa Malkia, England kwa kipigo cha 2-1 na kuwafuata mabingwa wa Kombe hilo wa mwaka 1998, Ufaransa walioing’oa Ubelgiji 1-0, mfungaji akiwa ni Samuel Umtiti.

Moscow, Russia. Fainali za Kombe la Dunia 2018, zilizoanza kutimua vumbi, Juni 14,  mwaka huu, zitamalizika Jumapili hii kwa mechi ya kibabe ya fainali, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Russia, maarufu kama Luzhniki na kushuhudiwa na mashabiki 81, 000 pamoja na wengine wengi kutoka kila pembe ya dunia.
Croatia maarufu kama ‘Watoto wa Mama’, walitinga hatua hii ikiwa kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa lao, baada ya kuwazima wajukuu wa Malkia, England kwa kipigo cha 2-1 na kuwafuata mabingwa wa Kombe hilo wa mwaka 1998, Ufaransa walioing’oa Ubelgiji 1-0, mfungaji akiwa ni Samuel Umtiti.
Kwa kuiangalia Croatia jinsi ambavyo wamekuwa wakifanya tangu mechi yao ya kwanza, Mwanaspoti inakuchambulia sababu kuu tatu zitakazoibeba Croatia dhidi ya Ufaransa pale Luzhniki mbele ya mashabiki 81,000 akiwemo Rais wao Mwanamama, Madam Kolinda Grabar-Kitarović.

1. Umoja na utulivu ndani ya kikosi pamoja na hamasa ya mashabiki
Kocha wa Croatia, Zlatko Dalic amefanya maajabu katika kikosi chake. Amehakikisha kikosi kinakuwa na mshikamano. Kikosi cha Croatia kinaishi kama ndugu. Kuanzia kwa Rais wao hadi nahodha wao, wote wanapendana kinoma.

2. Utulivu wa kiakili na nidhamu ya mchezo
Mechi tatu dhidi ya Denmark, Russia na England, ilishuhudia Croatia ikitoka nyuma na kupata ushindi. Mechi mbili kati yao, ilienda kwenye hatua ya matuta. Wameonesha ubabe na moyo wa kupambana balaa. Ushindi walioupata dhidi ya England, ulihitaji moyo wa kujituma.
Nahodha wao Luka Modric, amenukuliwa mara nyingi akisema: "Tumeonesha tabia halisi ya Wacroatia, hatukati tamaa. Ni ngumu kushinda mechi bila nidhamu ya mchezo, kila siku kocha amekuwa akisisitiza nidhamu ndani na nje ya uwanja."

3. Uzoefu na Kujiamini
Kama kuna timu inayojiamini ni Croatia. Kwanza wana watu wenye pesa zao nyuma yao, akiwemo 'mama yao'. Pili wanapesa na tatu wana uzoefu. Kikosini kuna majina kama Luca Modric, Ivan Rakitic, Mateo Kovacic, Dejan Lovren. Rebic, Ivan Perisic na Mario Mandzukic, bila kumsahau kipa wao Dejan Subasic