#WC2018: Rais wa FIFA afagilia Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Mpaka sasa mechi 62 zimeshachezwa ambapo kati ya mataifa 32 yaliyokita kambi nchini Russia kutafuta ufalme wa soka duniani, ni Ufaransa na Croatia tu zilizosalia, huku England na Belgium nazo zikitarajiwa kumalizana katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu.

Moscow, Russia. Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino ameifagilia michuano ya mwaka huu ya Kombe la Dunia, yanayoingia fainali Jumapili hii itakayokutanisha Ufaransa na Croatia kwenye dimba la Luzhniki.

Mpaka sasa mechi 62 zimeshachezwa ambapo kati ya mataifa 32 yaliyokita kambi nchini Russia kutafuta ufalme wa soka duniani, ni Ufaransa na Croatia tu zilizosalia, huku England na Belgium nazo zikitarajiwa kumalizana katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu.

Akizungumzia mwenendo wa mashindano bosi huyo wa soka aliwashukuru Warusi kwa kuandaa michuano aliyoyataja kuwa bora zaidi kuwahi kutokea na kuongeza kuwa anatarajia Qatar watakuja na kitu kipya na bora kuliko ilivyokuwa mwaka huu.

"Kwa muda mrefu nilisema hii itakuwa ni michuano babkubwa, sasa nadhani kila mtu amejionea. Mataifa yaliyotabiriwa kutamba yamerudi nyumbani, ushindani ulikuwa mkali, mazingira yalikuwa mazuri, tunatarajia kushuhudia makubwa kutoka kwa Qatar mwaka 2022," alisema Infantino na kuongeza.

 

 

"Ahsanteni sana watu wa Russia, ahsante sana Rais Putin na watu wako, kwa kweli mmetuonesha jinsi soka linavyoweza kuunganisha watu. Ahsante sana kwa kamati ya maandalizi, shirikisho la soka la Russia, na kila mtu aliyehusika kuhakikisha michuano hii inakuwa ya kivutia."

Michuano hii inatarajiwa kuweka tuo, Jumapili hii pale Bingwa atakapopatikana baada ya Ufaransa na Croatia kutoa jasho katika uwanja wa Luzhniki mbele ya mashabiki 81,000 kwa kufuata amri na maelekezo ya pilato wa siku hiyo, Nestor Pitana wa Argentina