#WC2018: Nchi zenye mashabiki wengi Russia 2018

KOMBE la Dunia 2018 linazidi kuwapa burudani mashabiki wa soka duniani kote. Mambo ni moto na kila siku kuna matukio mapya yanayopendezesha michuano hiyo. Jambo hilo ndio maana limefanya michuano hiyo kuvutia mashabiki wengi kutoka kila pande ya dunia, waliokwenda Russia kushangilia. Ukiondoa wenyeji, nchi hizi sita ndizo zenye mashabiki wengi zaidi huko waliokwenda kushangilia fainali hizo.

6.Mexico-

asilimia 4.8

Mashabiki wa Mexico wamejazana huko Russia kwenye fainali za Kombe la Dunia kwenda kuishangilia timu yao na mambo yalikuwa mazuri kwao baada ya timu wanayoshabikia kuichapa Ujerumani kwenye mechi ya kwanza. Ni suala linalowapa hamasa kubwa wachezaji wa Mexico akiwamo Chicharito kwamba kuna kundi kubwa la mashabiki linatua Russia kuwashangilia. Mexico inamiliki asilimia 4.8 ya mashabiki wote waliopo Russia kwa sasa.

5.Korea Kusini-

asilimia 5.1

Korea Kusini walifanya kila wanaloweza kupata pointi kwenye mechi yao ya kwanza dhidi ya Sweden, lakini kucheza kizembe kuliwafanya wasababishe penalti iliyowagharimu na kupoteza mechi hiyo. Jambo hilo liliwauma sana kwa sababu Korea ni moja ya nchi zilizokwenda na mashabiki wengi kwenye fainali hizo za Russia. Hakika sasa, watalazimika kupambana kweli kweli kwenye mechi zake zijazo. Korea ina mashabiki asilimia 5.1 kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia huko Russia.

4.Argentina- asilimia 5.6

Unaweza kuona ni maumivu makali kiasi gani Lionel Messi na wenzake wanawasababishia mashabiki wao waliopo kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia. Hadi sasa kikosi hicho kimeambulia pointi moja tu, huku wakikabiliwa na mechi ngumu sana ya mwisho kwenye kukamilisha hatua ya makundi wakitarajia kumenyana na Nigeria. Argentina, yenye mashabiki asilimia 5.6 kati ya wote waliopo Russia kwa sasa, imetoka sare na Iceland kisha ikaja kufungwa 3-0 na Croatia.

3.Hispania- asilimia 5.8

Hispania ilianza kwa sare kisha ikapata ushindi mwembembe sana mbele ya Iran katika mechi yao ya pili kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia. Mabingwa hao wa dunia wa mwaka 2010 waliwapa imani kubwa mashabiki wao na ndio maana wameenda kwa wingi huko Russia kushangilia, ambapo inamiliki asilimia 5.8 ya mashabiki wote. Mechi yao ya mwisho watacheza na Morocco, hivyo watahitaji sana kusonga mbele kuwafanya idadi hiyo ya mashabiki waendelee kuwapo Russia au kuongezeka kabisa.

2.Brazil- asilimia 6.6

Brazil ilianza kampeni zake za kusaka ubingwa wa dfunia kwa sare ya 1-1 dhidi ya Uswisi kabla ya kuja kuichapa Costa Rica 2-0 kwenye mechi ya pili. Ingekuwa kitu cha ajabu kama ingeshindwa kufanya vizuri kwenye mechi hiyo ya pili hasa ukizingatia kwamba Brazil ni moja ya timu mbili za juu zenye mashabiki wengi kwenye fainali hizo za Russia ukiweka kando wenyeji. Brazil inamiliki asilimia 6.6 ya mashabiki wote waliopo kwenye fainali hizo za Russia.

1.Marekani- asilimia 12.4

Marekani haijafuzu Kombe la Dunia 2018, lakini hilo halijawafanya mashabiki wa taifa hilo tajiri duniani kwenda Russia kushangilia michuano hiyo. Takwimu zinaonyesha kwamba Marekani inamiliki asilimia 12.4 ya mashabiki wote waliopo kwenye fainali hizo na wanachofanya wao ni kushangilia tu timu inayowapendeza kufanya hivyo.