Vigogo wengine TFF kizimbani

Muktasari:

Hata hivyo, Mahakama hiyo ya Kisutu itaanza kusikiliza kesi hiyo kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka kuanzia Mei 14,17 na 21, mwaka huu.

MENEJA wa Ofisi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya wameunganishwa katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 inayomkabili aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi na wenzake wawili.

Hata hivyo, Mahakama hiyo ya Kisutu itaanza kusikiliza kesi hiyo kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka kuanzia Mei 14,17 na 21, mwaka huu.

Washtakiwa hao wameunganishwa katika kesi hiyo jana kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri mara baada ya Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai kuomba kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka na mahakama kuridhia.

Baada mahakama kuridhia washtakiwa walisomewa mashtaka 30 badala ya 28 yaliyokuwa yakiwakabili awali Malinzi (57), Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine (46) na Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga (27).

Katika mashtaka hayo, Malinzi anakabiliwa na mashtaka 28 ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa USD 173,335 naSh 43,100,000.

Mwesigwa anakabiliwa na mashtaka sita ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi na utakatishaji wa fedha.

Kwa upande wa Nsiande anakabiliwa na mashtaka mawili ya utakatishaji wa fedha, mshtakiwa Zayumba yeye anakabiliwa na mashtaka tisa ya kughushi na Flora anakabiliwa na shtaka moja la kughushi.

Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka hayo walikana na upande wa mashtaka ukadai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na wakaomba kuwasomea washtakiwa hao maelezo ya awali (PH).

Baada ya kusomewa maelezo ya awali, washtakiwa wote walikubali maelezo yao binafsi na hata hivyo, Zayumba na Flora walipata dhamana kwa sababu mashtaka yanayowakabili yanadhaminika.

Flora aliachiwa kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.