Upepo wa Pogba wahamia Barcelona

London, England. Siku za kiungo nyota, Paul Pogba kubaki Manchester United zinahesabika baada ya wakala wake Mino Raiola kuongeza kasi ya kutaka nyota huyo ajiunge na Barcelona.

Raiola, mmoja wa wakala maarufu duniani, amemtaka mchezaji huyo wa Ufaransa kuondoka Man United kabla ya dirisha la usajili kufungwa Agosti 9.

Wakala huyo alizungumza na Barcelona na muda mfupi ujao anajipanga kuteta na Man United kuhusu mchakato huo.

Kocha Jose Mourinho hakuwa na uhusiano mzuri msimu uliopita na wakala huyo anataka kutumia fursa hiyo kumpeleka Barcelona.

Wakati Raiola akitaka Pogba kutimkia Barcelona, Man United imesema kiungo wa kimataifa wa Ufaransa hauzwi katika usajili wa majira ya kiangazi.

Juzi, Barcelona iliweka mezani Pauni 44.6 na kutoa wachezaji wawili Yerry Mina ama Andre Gomes, lakini Man United iliweka ngumu.

Wakala huyo ana hofu kama Pogba atacheza kwa kiwango bora msimu ujao baada ya kuibua mzozo wa mara kwa mara na Mourinho.

Man United imeingia hofu ya kumpa mshahara mkubwa unaofikia Pauni500,000 kwa wiki sawa na Alexis Sanchez.

Chanzo ndani ya Man United kimedokeza Raiola ameongeza presha ya mchezaji huyo kuondoka ili kushinikiza mteja wake kuingia mkataba mpya utakaompa dau kubwa la mshahara.