Uhuru Suleiman amvuruga Kocha Biashara United

Muktasari:

  • Biashara United iliyopanda Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza, ilianza msimu kwa kasi na kuifunga Singida United ugenini bao 1-0, na baada ya hapo, walipoteana na kufungwa mechi mbili mfululizo na Coastal Union 1-0, na Stand United 1-0.

Musoma. Kocha Mkuu wa Biashara United ya Mara, Hitimana Thiery amesema, wachezaji Uhuru Suleiman na Mpapi Nassib wanaweza kuwa sababu ya timu hiyo kukosa pointi tatu katika mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar.

Uhuru na Mpapi hawakucheza mechi hiyo wakalazimishwa suluhu katika uwanja wao wa nyumbani wa Kumbukumbu Karume mkaoni Mara, matokeo yaliyowaweka kwenye nafasi ya 11 na pointi nne.

Hitimana amesema, wachezaji hao walishindwa kucheza kwa sababu ya  matatizo ya kifamilia jambo lililofanya safu ya ushambuliaji kupwaya.

Amesema, wachezaji wake walipambana lakini ushindani ulikuwa mkubwa na sasa wanajipanga kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Azam.

“Mchezo ulikuwa mgumu lakini nimeona makosa safu ya ushambuliaji ambapo kulipwaya na hii ni kutokana na kuwakosa Uhuru na Nassib,”alisema Thiery.