KWAKO MWL KASHASHA: Tusicheze mpira kwa hisia, tuangalie uhalisia

Muktasari:

Kandanda safi iliyochezwa na Stars hususani kipindi cha pili huko Benin kwenye ile mechi

HARAKATI za ujenzi wa Taifa Stars zinaendelea kutupa matumaini Watanzania, ni mwenendo mzuri kwa kiasi fulani lakini bado tunahitajika kuongeza bidii, hamasa, mikakati na mbinu za kuipa makali zaidi ya hivi ilivyo kwa kutumia kanuni ya nadharia katika kujifunza ya kutoka kwenye hali nyepesi kuelekea katika hali ngumu (from simple to complex operations).

Kandanda safi iliyochezwa na Stars hususani kipindi cha pili huko Benin kwenye ile mechi, limezidi kutoa picha halisi ya nini tunatakiwa kukifanya na kwa namna gani ili kupata majibu ya maswali na hoja nyingi mbalimbali kuhusu maendeleo endelevu na mafanikio ya Stars kwa siku za usoni.

Watanzania tunaendelea kusononeka kila linapokuja suala la viwango na ubora wa soka duniani na Afrika. Ni wazi kwamba hakuna mwananchi hususani mpenzi wa soka anayefurahi anaposikia au kusoma taarifa za kila mwezi za Fifa kwamba sisi tupo kwenye nafasi zaidi ya 100 na kuendelea, hii ni dalili ya kwamba kupata nafasi ya kushiriki fainali za Afcon au Kombe la Dunia bado ni ngumu kwa sababu ni nadra sana nchi iliyopo katika nafasi zaidi ya 100 katika viwango vya ubora wa kandanda kucheza fainali hizo.

Kwa upande wa Afrika nchi ikiwa nje ya 20 bora ni vigumu pia kucheza Afcon ikitokea basi ni mara chache kama ilivyokuwa kwa Zimbabwe iliyoshiriki fainali za Afcon za Gabon ikiwa nafasi ya 28.

Pongezi kwa TFF kwa kufanikiwa kupata mechi ya kimataifa safari hii kwa kucheza na moja ya mataifa kutoka Afrika ya Magharibi ili kuwapa wachezaji wetu uzoefu wa kupambana na timu ngumu kwa lengo la kujifunza zaidi na kukomaa kimataifa.

Mechi yetu na Benin , Tanzania tulikuwa nafasi ya 136 na wenzetu nafasi ya 79, ikiwa na maana kwamba kulikuwa na tofauti ya nafasi 57, hili ni pengo kubwa sana kati yetu tuna kila sababu ya kuwaheshimu wapinzani wetu.

Binafsi mchezo dhidi ya Benin ulikuwa mzuri kwa mantiki ya uwezo wa wachezaji wetu wote ,juhudi binafsi na nidhamu kwa jumla. Sambamba na hayo, lakini pia matokeo tuliyoyapata ya bao 1-1 hayakuwa mabaya ukizingatia kwamba ilikuwa ni mechi ya ugenini na laiti kama mwamuzi angetenda haki timu yetu ingeondoka na ushindi kwa asilimia 100.

Kiufundi timu yetu pamoja na kiwango inachokionesha inazo sura mbili ambazo watendaji katika Shirikisho kwa kushirikiana na benchi la ufundi watahitaji kuendelea kuzifanyia kazi, sura ya kwanza ni kucheza mpira kwa hisia badala ya hali halisi ilivyo kiwanjani na sura ya pili ni tabia ya wachezaji kuridhika na kujihami zaidi kitu ambacho kimetufanya kupata sare au ushindi mwembamba katika mechi nyingi ambazo hatukustahili kupata sare au kukosa ushindi mnono.

Tunapoteza nafasi nyingi za wazi, hapa kuna mambo ya kuyatazama kiufundi, mbinu, kisaikolojia na utawala (aina ya maandalizi).

Katika pambano la juzi, mengi yamesemwa na kuainishwa kama sehemu ya kile tulichokiona, mara nyingi timu yoyote inafanya kazi kwa kuzingatia misingi kadhaa ambayo inatengeneza umbo na muonekano wake kuwa mzuri au mbaya, Stars ya juzi huko Benin ilionyesha kwa kiwango kizuri cha utendaji mambo mengi au machache yafuatayo:

Kwanza, umoja;-Timu yetu ilionekana ina umoja na ushirikiano wakati wote kwa sababu walimudu kukabiliana na changamoto mbali mbali za ugenini ili wapiganie bendera yetu na sifa ya nchi kwa ujumla wake

Pili, nidhamu ya mchezo;-Mara baada TFF kutangaza kwamba timu yetu itasafiri kwenda kucheza na Benin, ziliibuka hisia na mawazo kwamba huenda mchezo ungekuwa mgumu sana kwetu na labda tungepoteza kutokana na kwenda kucheza ugenini tena timu yenye kiwango bora zaidi kuliko sisi,lakini kwa tahimini ya jumla timu ilikuwa na nidhamu ya hali ya juu na ilionekana kucheza kwa kufuata maelekezo ya benchi la ufundi, muda mwingi kulikuwa na ulinganifu na uwiano mzuri katika idara zote (team balance),hali iliyowasaidia kutotoa mwanya kwa wapinzani kucheza wanavyotaka.

Tatu, uwezo binafsi wa wachezaji;-Kwa jumla, kila mchezaji aliyepata nafasi ya kucheza alionekana yupo vizuri kwa maana ya kumiliki mpira mguuni lakini na uwezo wa kucheza na wenzake kwa kupiga pasi fupi fupi na ndefu kulingana na mazingira ya mchezo,hali ya mchezo na mahitaji ya kiufundi,zilikuwepo kasoro ndogo ndogo za kupoteza mipira lakini walijitahidi kurekebisha haraka kabla ya kusababisha madhara kwenye lango lao.

Nne, wachezaji wa kulipwa;-Uwepo wa wachezaji wa kulipwa katika timu ya taifa kuna mchango mkubwa uwanjani, licha ya timu yetu katika mchezo ule kuwa nao wachezaji watano tu lakini msaada wao ulionekana katika mambo mengi ikiwa ni pamoja na kucheza kwa kujiamini na kujitambua hasa pale timu inapokuwa kwenye  wakati mgumu.

Kimsingi, tunahitaji kuendelea kufanya juhudi za makusudi kuongeza idadi ya wachezaji wa kulipwa nje ya nchi watusaidie kuimarisha taifa stars.

Mwaka unaelekea ukingoni kukamilika, TFF na wadau wengine wote wa soka nchini tutumie nafasi ya mwezi mmoja uliosalia kutafuta mechi nyingine ya kimataifa kubwa zaidi ya Benin ili tuone mwisho wa 2017 timu yetu itakuwa na mwelekeo wa kiwango gani ,hiyo iakuwa ni dira kwa ajili ya benchi la ufundi na washirika wengine wote kupanga na kutayarisha mikakati ya mwakani kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunajinasua kwenye nafasi mbaya na tusiyostahili kuwepo katika ubora wa kiwango cha kucheza mpira Afrika na duniani kwa ujumla.