Try Again avunja ukimya Msimbazi

Muktasari:

  • Maneno hayo ya Salim ‘Try Again’ ikiwa ni mahojiano maaluma na Mwanaspoti likitaka kujua mambo mbalimbali kuhusu Simba hasa katika kipindi cha uongozi wake kitakachotamatika mara baada ya uchaguzi ambao mchakato wake unaendelea kwa kasi kukamilika.

KHATIMU NAHEKA

“Simba bado ipo kwenye kipindi cha mpito kwa sasa, mwenendo wa mpango huu wa mabadiliko sio mbaya kulingana na muundo ambao tunautengeneza. Tunaposema kuna vitu vinakwenda kwa pamoja kwa maana ya timu na maendeleo ya klabu, hivyo sio kitu kibaya mpaka sasa tukiangalia mchoro wake iko vizuri.” Hayo ni maneno kutoka kwa Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah anavyoanza kuilezea klabu yake juu ya sasa ilipo.

Maneno hayo ya Salim ‘Try Again’ ikiwa ni mahojiano maaluma na Mwanaspoti likitaka kujua mambo mbalimbali kuhusu Simba hasa katika kipindi cha uongozi wake kitakachotamatika mara baada ya uchaguzi ambao mchakato wake unaendelea kwa kasi kukamilika.

Baada ya kuanza kwa kuelezea nafasi ambayo Simba ipo sasa kiungozi na mfumo, Try Again anaendelea kufafanua mambo muhimu kupitia mahojiano hayo yaliyodumu kwa dakika 46.

Mabadiliko yanaweza kuchukua muda gani?

Try Again anaeleza kuwa kwa uzoefu wake kutokana na alivyosimamia kwa nafasi kubwa akisema: “Unajua kuna mipango mingi ya klabu, lakini pia kuna mipango ya timu kwa maana ya kikosi, nitakufafanulia kila kimoja lakini ndani ya haya nitakayokuleza yanahitaji muda na ninavyoona mambo kuanza kuonekana kile kitu halisi ambacho tunaweza kukikusudia katika uwekezaji huu, inaweza kuchukua miaka mitatu hadi minne.

Mipango ya kikosi ikoje?

“Ukianza na mipango ya kikosi, eneo hili kuna mambo muhimu kwanza tunahitaji kutetea ubingwa wetu, lakini uongozi tunatambua kwamba baada ya kushiriki Kombe la Shirikisho msimu uliopita, msimu ujao tutashiriki Ligi ya Mabingwa.

“Uongozi tumeazimia lengo letu kubwa ni kufika hatua ya makundi hili ni lengo kubwa hatuwezi kusema tufike fainali ikitokea hivyo itakuwa sawa, lakini lengo kubwa ni kufika hatua ya makundi kwanza.

“Kufika hapo ngazi ya kwanza ndiyo kama hivi mnavyoona tumesajili timu bora na makocha wazuri ambayo tunaamini vyote kwa pamoja vitatufikisha pale tunapokusudia, tukifika hapo tunaweza kufikiria kuiboresha timu zaidi ili kwenda kufanya makubwa zaidi.

“Endapo tutafanikiwa kufika sehemu hii ambayo tunaikusudia sasa tutasajili timu bora zaidi itakayotufikisha hatua inayofuata huko katika fainali na na hata kuchukua kombe, lakini kwa sasa acha tuanze hapa.

Mipango YA klabu?

“Kwa upande wa maeneo kama klabu sasa huku kuna mambo mengi, moja ni uwanja, pili watendaji kwa maana sasa Simba inatambulika kama kampuni tutahitaji watendaji, kama mkurugenzi wa ufundi, mkurugenzi wa masoko, tutahitaji mkurugenzi wa fedha. Atahitajika Mtendaji Mkuu wa klabu, tutahitaji mtu mwenye taaluma ya kufanya uchambuzi ambao, hawa wote watarahisisha mambo ya kiuendeshaji na kuipa mafanikio klabu kupitia taaluma zao.

“Mipango ya kuwapata wote hao iko mbioni kuweza kuangalia tunaweza kuwapataje, gharama zao, wanapatikana wapi lakini una mipango mizuri zaidi kwa maana huenda kwa baadhi ya nafasi tunaweza tusipate watu mwafaka kulingana na vigezo vyetu.

“Tulichokubaliana tutachukua jukumu la kusomesha wazawa, pia ili wapate elimu na kuja kushika hizo nafasi na katika hili tunadhani tukiwasomesha wazawa tunaweza kupunguza gharama nyingi, hivyo mipango yote ndiyo maana nasema tunaweza kuanza kuona tunachoitaka katika Simba kuanza kuonekana baada ya muda huo wa miaka mitatu mpaka minne.

Wanachama wanaridhishwa na mfumo mpya?

“Unajua sio lazima kila mtakachofanya wanachama wote waridhike hasa mambo yanavyobadilika katika eneo fulani, hakuna kitu duniani watu wanaridhika kwa pamoja, kugongana kwa mawazo wakati fulani ni jambo zuri la kujenga kitu mnachopingana kiwe bora zaidi, hatuwezi kila kitu tukifanye na tukubaliane.

“Wakati tunaanza wapo waliokuwa wanapinga, lakini hatukuwabagua tulitumia nafasi yetu kuwaelewesha na baadaye sote tuliona wapo waliorudi tukawa pamoja na hata waliobaki bado tunawatambua kama sehemu ya kujenga, lakini kwa ujumla naona wanachama wanaridhika na jinsi mambo yanavyokwenda.

“Kitu kikubwa ambacho nakiona wanachama wanataka kuona timu yao inakuwa na mabadiliko kwa kupiga hatua, kama timu inafanya vizuri mambo mengine ambayo tunafanya kama uongozi inakuwa rahisi kuwaelewesha kwa utulivu na hatimaye kuubaliana.

Jukumu la kusimamia mabadiliko lilikuwaje?

“Halikuwa jepesi hata kidogo kwa sababu mfumo wenyewe ulivyakuwa umekaa, ulihitaji mtu mwenye nia thabiti ya kuhakikisha jambo hili linafanikiwa kwa maslahi ya wengi.

“Ilikuwa ni kazi ngumu kidogo, kwanza kuwaleta watu pamoja wakaelewa nini mnataka kufanya kwa namna gani.

“Tuliona ili watu waelewe vizuri tulikaa kuonyesha nia ya mafanikio kwa kuhakikisha timu kwanza inafanikiwa hilo likatupa wepesi kuwafikia wanachama kwa kutafuta watu maalum ambao, walitembea sehemu mbalimbali nchini kufikisha elimu ya mabadiliko na sasa tumefikia hapa.

“Kipekee niwashukuru sana kamati yangu ya utendaji nakumbuka kuna wakati tulikuwa tunafikia hatua ya kuzozana katika vikao, lakini bado sote tulitambua nia ni kuisaidia Simba tulieleweshana na kusimama wamoja. Kiukweli Kamati ya Utendaji imefanya kazi kubwa sasa kuifikisha hapa Simba ilipo.

Faida ya mabadiliko

“Faida ni kubwa kusema sana kwa sababu mabadiliko yanakwenda kuongeza uwezo wa klabu kwa maana sasa Simba itakuwa na fedha ambazo zitasaidia kufanikisha lolote, kuendesha klabu kubwa kama hii kunahitaji fedha, tunaamini mahitaji mengi yatapata ufumbuzi kutokana na mfumo utaavyokuwa unatengeneza fedha. Leo kama tunaweza kununua mchezaji kwa Dola 70,000 mpaka 100,000 huko mbele tunaweza kununua hata kwa Dola 500,000.

Siri ya mabadiliko

Baada ya mchakato wa mabadiliko kwenda kirahisi hapa, Try Again anaeleza siri ya mabadiliko hayo: “Siri kubwa ni mshikamano, upendo na misimamo thabiti, lakini pia kuweka uwazi wa mambo ambayo tulikuwa tunayafanya kwa maana ya mchakato mzima. Kama Kamati ya Utendaji tuliamua kusimamia hayo, lakini tulipata wepesi kutokana na utulivu wa wanachama wetu.

Kwanini hakuwania uongozi

“Ni uamuzi wa kidemokrasia. Inafahamika kwamba Simba ni klabu ya watu wengi, binafsi ninaamini wako wanachama wenzangu wengi wanatamani kuja kuweka michango yao katika klabu yetu. Mimi ni muumini wa demokrasia na nimeamua kutoa nafasi ili waje wapya kuendeleza pale nilipoishia, ningeweza kugombea na kupata nafasi yoyote kutokana na sifa nilizonazo na hata ushawishi, lakini kwa sasa sikuhitaji.

“Sababu ya pili kubwa niliona nikigombea nitakumbana na mgongano wa kimaslahi, kama mnavyojua nimehusika kutengeneza Katiba mpya ya klabu, nimeunda tume ya uchaguzi, nimesimamia mfumo wa mabadiliko lakini katika Katiba tukaweka vitu ambavyo ni vigezo vinavyoweza kutupa viongozi tunaowataka kwa hayo yote endapo ningegombea tungeneza tafsiri kuwa niliweka hayo yote ili nipate nafasi ya kugombea tena. Kuonyesha nia yetu ilikuwa, njema na kwa ajili ya kuijenga Simba na sio maslahi ya mtu binafsi, nikaona sababu hizo zinanitosha kuona nisigombee. Mimi bado kijana hakuna anayejua panapo uhai naweza kuja kuwania uongozi, lakini kwasasa ni vizuri niwaachie wengine.

Viongozi wenzake VIPI

“Katika historia ya maisha yangu huu ni uamuzi ambao ulinitaka niwe na msimamo mkali pengine kuliko wowote, nilipata presha kubwa kutoka kwa watu wangu wa karibu na hata mwekezaji mwenyewe. Wengi hawakutaka nifanye uamuzi kama huu, lakini unapokuwa kiongozi na ukajiamini lazima uwe na msimamo bila kutetereka. “Wapo waliotaka kunichukulia fomu, lakini msimamo wangu haukubadilika katika hili. Kuna wakati mambo kama haya yanaleta harufu ya rushwa kwa kuingiza viongozi kwa ushawishi wa fedha kitu ambacho sikukitaka katika uongozi wangu.

Je unafahamu nini kuhusiana na uwanja mpya wa Simba? Vipi kuhusu Simba mpya ya ndani na nje ya uwanja na mikakati ya kocha mwenye viwango vya juu kuifanya kutisha Afrika? Fuatilia mwendelezo wa makala haya kesho Jumamosi