TFF yatetea mechi 11 za Yanga Dar

Muktasari:

Ukosefu wa viwanja bora kwa klabu nyingi za Dar es Salaam umesababisha kutumia uwanja wa Uhuru au Taifa kila zinapocheza mechi zao za Yanga na Simba

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema hakuna upendeleo wowote kwa Yanga kama inavyozungumza kwa sasa na wadau wa soka.

Kauli hiyo ya TFF imekuja baada ya kuwepo madai kuwa Yanga imependelewa kucheza mechi zake 11 za Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wapenzi na wadau wa soka nchini walianza kuhoji juu ya michezo hiyo huku wakisema ratiba hiyo imeelekezea nguvu kwa Yanga pekee.

Akijibu madai hayo Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo alisema ratiba hiyo ipo sawa tofauti na watu wanavyoiangalia.

"Ratiba ipo sawasawa lakini kilichotokea ni kwamba Yanga wanacheza na timu za Dar es Salaam, kuna michezo hapa Yanga wapo ugenini, lakini wanaonekana kama hawajatoka lakini ni ratiba na wapo ugenini nao," alisema.

Michezo watakayocheza Yanga wakiwa Dar, Yanga vs Stand Utd, Yanga vs Coastal, Yanga Vs Singida, Jkt Tanzania Vs Yanga, Simba Vs Yanga, Yanga vs Mbao, Yanga Vs Alliance, KMC Vs Yanga, Yanga vs Lipuli, Yanga vs Ndanda na African Lyon dhidi ya Yanga.