TFF yamuomba Rais Magufuli aikabidhi kombe Simba

Wednesday May 16 2018

 

By Eliya Solomon, Thomas Ng’itu mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka nchini (TFF), limepeleka ombi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Magufuli likimtaka kuikabidhi Simba, Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Jumamosi katika mchezo utakaoikutanisha timu hiyo na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Mbali na kuikabidhi Simba, kombe hilo, Rais Magufuli pia atakabidhiwa Kombe la Ubingwa wa Vijana wenye umri chini ya miaka 17 kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati. Timu ya taifa ya vijana wa umri huo (Serengeti Boys) ililitwaa ubingwa nchini Burundi mwezi uliopita.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia alisema shirikisho hilo limepeleka ombi hilo maalum kwa Rais Magufuli, kwa lengo la kumuonyesha jinsi mpira wa miguu unavyounga mkono kwa vitendo, sera yake ya kujenga uchumi.

“Tumemuomba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Magufuli awe mgeni rasmi katika kupokea Kombe la Afrika Mashariki na Kati kutoka kwa vijana wetu wa Serengeti Boys, ambalo walilichukua kule Burundi, lakini vile vile awakabidhi Simba, Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Kufika kwake ni jambo kubwa sana. Mpira ni moja ya viwanda na tukumbuke kwamba Rais wetu anataka uchumi wa viwanda,” alisema Rais Karia.

Aprili 29, Serengeti Boys ilitwaa Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati kwa vijana wenye umri usiozidi miaka 17, baada ya kuifunga Somalia kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa fainali huko Burundi.

Kabla ya hapo, Serengeti Boys iliifunga Kenya mabao 2-1 katika hatua ya nusu fainali ambayo walifuzu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Sudan na kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi za hatua ya makundi.

Simba yenyewe imetwaa Ubingwa wa Ligi Kuu, baada ya kukusanya pointi 68 ambazo hazitoweza kufikiwa na timu nyingine yoyote katika Ligi Kuu inayotarajiwa kufikia tamati, Mei 31.