Stand United: Huyo Makambo atafute pa kucheza

Muktasari:

Yanga haijawahi kufungwa na Stand United kwenye Uwanja wa Taifa au Uhuru, Dar es Salaam

Mwanza. Kocha msaidizi wa Stand United, Athumani Bilali ‘Bilo’ amesema wamejiandaa vilivyo kumkabili mshambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo watakapokutana naye Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kocha Bilo alisema anajua uimara ya safu ya ushambuliaji inayongozwa na Makambo, lakini wamejipanga kuhakikisha Straika huyo hatafurukuti katika mchezo huo.

Alisema wamewapa kazi maalumu mabeki wao kuhakikisha Straika huyo raia wa DR Congo hachezi kabisa Jumapili kwani wanajua ndio injini yao kwa sasa.

“Tunajua uimara wa safu ya ushambuliaji Yanga na tunajua Makambo ndio wanaomtegemea hivyo tumejifua vya kutosha na watamwonea huruma mashabiki wao kwani hatofurukuta,”alisema Bilo.

Kocha huyo alisema katika kipindi hichi cha mapumziko wameweza kujifua vya kutosha ambapo kikosi chao kimeimarika haswa katika safu ya ushambuliaji iliyokuwa butu.

“Tulikuwa na mapungufu katika safu ya ushambuliaji, lakini tayari tusharekebisha hizi kasoro washambuliaji wetu walikuwa wanakosa umakini wanapofika langoni na kusababisha tukose mabao ya wazi,”alisema kocha huyo.

Stand United ina pointi sita baada ya kucheza mechi tatu ambapo iliwatandika African Lyon bao 1-0 kisha ikachapwa na Mbao FC mabao 2-1 na wakaitandika Biashara United bao 1-0.