Simba wanne, Yanga watatu tuzo Mchezaji bora

Muktasari:

  • Imebakia kuduchu kutangazwa mchezaji bora

Dar es Salaam. Nyota wanne wa Simba na watatu wa Yanga ni miongoni mwa wachezaji 15 waliopita katika mchujo wa kwanza wa kuwania tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka Tanzania Bara katika sherehe zinatarajia kufanyika Juni 23, kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Kamati ya Tuzo za ligi kuu Bara imetangaza majina ya wachezaji 15 kati ya 30, ili kupata watatu watakaowania tuzo ya mchezaji bora wa msimu 2017/18.

Katika orodha hiyo ya wachezaji 15, Simba imeingiza majina manne nahodha John Bocco, Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya na Erasto Nyoni huku Yanga wakiwa ni Obrey Chirwa, Papy Tshishimbi na Kelvin Yondani.

Wachezaji hao 15 na majina ya timu zao katika mabano ni Obrey Chirwa, Papy Tshishimbi na Kelvin Yondani (Yanga),  Shafiq Batambuze, Mudathir Yahya na Tafadzwa Kutinyu (Singida United), Wengine ni Adam Salamba (Lipuli), Habibu Kyombo (Mbao), John Bocco, Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya na Erasto Nyoni (Simba), Marcel Kaheza (Majimaji), Yahya Zayd (Azam) na Hassan Dilunga (Mtibwa).

Kamati ina kazi nzito ya kupunguza idadi ya wachezaji 15 mpaka kufikia watatu ambao watatangazwa wiki ijayo, hatua hiyo itawahusisha  wahariri wa habari za michezo, manahodha wa timu za Ligi Kuu na makocha.

Pia kutatolewa tuzo mbalimbali ya Bingwa wa VPL, Mshindi wa Pili, Mshindi wa Tatu, Mshindi wa Nne na Mfungaji Bora.

Tuzo nyingine ni Timu yenye Nidhamu Bora, Mchezaji Bora wa Ligi ya Vijana (Tuzo ya Ismail Khalfan), Mchezaji Bora Chipukizi, Mwamuzi Msaidizi Bora, Mwamuzi Bora, Kipa Bora, Kocha Bora, Goli Bora, Kikosi Bora cha Msimu na Mchezaji wa Heshima.