Simba hii haiachi kitu! Hodi Mtwara

Muktasari:

  • Simba wamesafiri na jumla ya wachezaji 20 huku nane wakibaki na wataendelea na mazoezi chini ya kocha msaidizi Masoud Djuma wakichanganyika na wachezaji kutoka timu ya vijana (U-20).

Mtwara. Kikosi cha Simba kimeasili Mtwara leo Alhamisi kwa ajili ya mechi ya mzunguko wa tatu wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda.

Simba wamesafiri na jumla ya wachezaji 20 huku nane wakibaki na wataendelea na mazoezi chini ya kocha msaidizi Masoud Djuma wakichanganyika na wachezaji kutoka timu ya vijana (U-20).

Wachezaji waliobaki ni Yusuph Mlipili, Ally Salim, Rashid Juma, Abdull Selemani, Said Nduda, Asante Kwasi na Mzamiru Yassin.

Simba wanaingia katika mechi na Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona huku wakiwa hawana rekodi ya kupoteza katika uwanja huo wala kufungwa na Ndanda tangu walivyopanda Ligi 2015.

Kikosi cha Simba huenda kikakamilika na kuimarika zaidi baada ya kulejea kwa Juuko Murshid ambaye aliondoka nchini bila ya kuwa na maelewano mazuri na Uongozi wa Simba.

Habari njema kwamba Juuko ameshamalizana na Uongozi wa Simba na muda wowote kuanzia sasa atajiunga na katika programu za timu.

Kurudi kwa Juuko katika kikosi cha Simba kuyafanya kuwa na mabeki wa kati saba ambao ni Mlipili, Poul Bukaba, Erasto Nyoni, James Kotei, Pascal Wawa na Salim Mbonde ambaye anaendelea kuuguza maumivu ya goti.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems baada ya kupata taarifa za kurudi kwa Juuko hazikuwa za kushangaza kwake kwani alitegemea hilo baada ya kumuona katika mechi na Uganda dhidi ya Taifa Stars.

Aussems alisema kama unakumbuka nilishakuambia awali mara baada ya mechi ya Stars kumalizika kuwa Juuko beki mzuri ambaye nitawaambia viongozi wamalize tofauti naye ili arudi katika kikosi.

Anasema nashukuru wamelifanikisha hilo na jukumu litabaki katika mikono yangu kumtumia kwa aina ya mechi gani.

"Kwanza kufika kwake ndani ya timu ni hatua kubwa ambayo imefanyika lakini nataka kwanza kumuona akifanya mazoezi chini yangu ili kumuona na kufahamu ubora wake," alisema.

"Kuhusu nitamtumia kwa aina gani au kama nitapangua ukuta wa wachezaji ambao wameshacheza mechi za mwanzo hilo lipo chini yangu na ambaye atakuwa bora katika hao ndio atapata nafasi ya kucheza.

"Mabeki wote wa kati wapo hapa ni wazuri na najivunia kuwa na wachezaji wanaofanya kazi yao kwa umakini kwani muda mwingine huwa sipati wakati mgumu kupanga wa kucheza katika eneo hilo kwani wote wapo vizuri.

"Juuko kama ataonyesha kiwango ananafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza kwani msimu huu tutakuwa na mechi nyingi kwahiyo sina shaka kwa matumizi yao na kama ikishindikana kabisa watakuwa wakicheza kwa kupishana," alisema Aussems.

Daktari naye yumo

Mabosi wa Simba katika kuhakikisha wanatokomeza tatizo la majeruhi wamemleta daktari Joseph Msaka kutoka Tanga atakayekuwa akisaidiana na Yassin Gembe.

Gembe alisema shida kubwa ya wachezaji wao kupata majeruhi ni kucheza mechi nyingi mfululizo ndio maana msimu huu wamefanya usajili wa kutosha ili akikosekana mmoja pengo lake awepo wa kuziba.

"Kingine mara nyingi huwa tunatumia viwanja vigumu ambavyo huzakisha majeruhi kwa wachezaji wengi lakini pia mpira ni mchezo wa kugusana na kushindana lolote linaweza kutokea.

"Lakini kwa kushirikiana na mwenzangu huyu naimani tutafanya kazi vizuri na kwa kushirikiana ili kuhakikisha wachezaji wetu wote wanakuwa Sawa katika kila mechi," alisema Gembe.