Samatta aupiga mwingi balaa

Monday April 9 2018

 

By ELIYA SOLOMON

NAHODHA wa Taifa Stars,Mbwana Samatta amekuwa shujaa kwa kuiongoza vyema klabu yake ya KRC Genk ya Ubelgiji kulipa kisasi cha bao 1-0 dhidi ya Standard Liège.

Machi 17, KRC Genk ilifungwa katika dakika thelathini za nyongeza bao 1-0 na Standard Liège kwenye fainali ya Kombe la FA (Cofidis Cup) baada ya kutoka suluhu ndani ya dakika 90.

Samatta ambaye alianza kwenye kikosi hicho cha Genk hapo juzi kwenye mchezo wa Ligi Kuu nchini humo, alikuwa mwiba wa kuotea mbali kwa kuwatesa, Luyindama Nekadio na Konstantinos Laifis ambao walikuwa wakimkaba.

Samatta ambaye alipiga mashuti manne kwenye mchezo huo, alikuwa sehemu ya upatikanaji wa bao lao kwa kufanyiwa madhambi na beki wa kushoto wa Standard Liège, Pocognoli kwa kumsukuma kwenye eneo la hatari.

Mwamuzi wa mchezo huo, Van Driessche alipuliza kipyenga na kuwapa Genk penalti iliyowapatia bao lao la ushindi dakika ya 49 lililofungwa na Leandro Trossard.

Takwimu za mchezo huo,zimeonyesha Samatta alikuwa na usahihi wa pasi zake kuwafikia walengwa kwa asilimia 88,aligusa mipira mara 32 huku akitengeneza nafasi mbili za wazi.