Saba tu ndo wapo salama Man United

Muktasari:

Ripoti zinadai kwamba Mourinho amepanga kuwaondoa mastaa wengi kwenye kikosi chake, lakini kuna saba hao wameripotiwa sura zao zitaendelea kuonekana kwenye kikosi cha wababe hao wa Old Trafford msimu ujao.

MANCHESTER, ENGLAND

HABARI ndiyo hiyo. Kinachodaiwa kuna idadi ya wachezaji saba tu kwenye kikosi cha Manchester United ambao wapo salama wasikumbwe na fagio la Jose Mourinho mwishoni mwa msimu huu.

Ripoti zinadai kwamba Mourinho amepanga kuwaondoa mastaa wengi kwenye kikosi chake, lakini kuna saba hao wameripotiwa sura zao zitaendelea kuonekana kwenye kikosi cha wababe hao wa Old Trafford msimu ujao.

Mreno huyo atahakikisha kuna usalama mkubwa unaowahusu mastaa wake David De Gea, Alexis Sanchez, Romelu Lukaku, Nemanja Matic, Jesse Lingard, Ashley Young na Juan Mata wanaendelea kubaki kikosini mwa miamba hiyo ya Old Trafford. Hao ndio wachezaji ambao Mourinho anaonekana kuwa na imani nao.

Taarifa za kutoka Old Trafford zinadai Mourinho anatazama zaidi wale wachezaji ambao wamekuwa wakimpa matokeo mazuri kwa siku za karibuni, lakini bado kumekuwa na wasiwasi mkubwa juu ya kiungo ghari zaidi, Paul Pogba.

Hata hivyo, inadaiwa mpango wa usajili wa Mourinho unabadilika mwezi hadi mwezi na baada ya mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Tottenham Hotspur kunaweza kuwa na mabadiliko mengine ambayo kocha huyo ataibuka nayo kwenye kuhakikisha msimu ujao anatengeneza kikosi cha ushindi kupambana na Manchester City katika mbio za kusaka ubinvgwa.