Parlour ampeleka Benitez Arsenal

Muktasari:

  • Makocha mbalimbali wameanza kupigana kikumbo kuwania nafasi ya Wenger ambaye ametangaza kuachia ngazi mwishoni mwa msimu huu.

London, England. Nyota wa zamani wa Arsenal, Ray Parlour, amemtaja kocha Rafael Benitez kuwa ana sifa ya kujaza nafasi ya Arsene Wenger.

Makocha mbalimbali wameanza kupigana kikumbo kuwania nafasi ya Wenger ambaye ametangaza kuachia ngazi mwishoni mwa msimu huu.

Mfaransa huyo ameinoa Arsenal kwa miaka 22 tangu alipotua Emirates kutoka Monaco ya Ufaransa mwaka 1996.

Kiungo huyo wa pembeni aliyecheza kwa mafanikio Arsenal alidokeza Benitez ni kocha bora mwenye uwezo mzuri katika medani ya soka.

Parlour aliyecheza katika kikosi kilichoundwa na nyota mbalimbali kina Patrick Vieira na Thierry Henry, alisema vigogo wa Arsenal hawana sababu ya kusaka kocha mpya zaidi ya Benitez.

“Kazi nzuri aliyofanya Newcastle msimu huu imewashangaza wengi, haina uwekezaji mkubwa lakini timu inacheza kwa kiwango bora, Newcastle ipo salama katika msimamo wa ligi,” alisema nguli huyo.

Kocha wa zamani wa Barcelona Luis Enrique anapewa nafasi kubwa ya kutua Arsenal.