Ngassa, Makambo wapagawisha kinoma Yanga

Muktasari:

  • Martin alisema Makambo anaonekana ni fundi wa kuzifumania nyavu na kwamba ana kasi ya ajabu, akidai kuwa akifanya hivyo kwenye ligi inayoanza Agosti 22 basi Yanga itakuwa imepata mtambo wa mabao kama ilivyokuwa kwa Obrey Chirwa.

Dar es Salaam.Winga wa Yanga, Emmanuel Martin amesema  Mrisho Ngassa na Heritier Makambo wameongeza nguvu kwenye kikosi hicho kutokana na ufundi wao mazoezi huko mkoani Morogoro ambako wameweka kambi kujiandaa na mechi dhidi ya MC Alger, michuano ya Shirikisho pamoja na ligi kuu.

Martin alisema Makambo anaonekana ni fundi wa kuzifumania nyavu na kwamba ana kasi ya ajabu, akidai kuwa akifanya hivyo kwenye ligi inayoanza Agosti 22 basi Yanga itakuwa imepata mtambo wa mabao kama ilivyokuwa kwa Obrey Chirwa.

"Kwa upande wa Ngassa ni mchezaji mzoefu na hajaisha kama watu wanavyomchukulia, nadhani akiwaliza kwenye ligi ndipo watakapompa saluti, naamini wawili hao kwa safu ya mbele watafanya kitu kikubwa,"alisema.

Mbali na hilo alisema wapo fiti kwa ajili ya kuwakabili MC Alger, Agosti 19 na kwamba watapumzika siku tatu kisha wataenda kuvaana na Mtibwa Sugar kwenye mechi ya ligi kuu, ambapo wataanzia ugenini.

"Tumejiandaa kikamilifu, naamini tutafanya vizuri kwani akili zetu kwa sasa zipo imara kwa ajili ya kukabiliana na ushindani wa wapinzani wetu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

"Baada ya mchezo huo tutapumzika siku tatu, kujiandaa na mechi ya ligi kuu na Mtibwa Sugar, hivyo mashabiki wetu watuamini kwamba tutafanya vizuri kwa mechi zote mbili,  wasiache kutuunga mkono,"alisema.