Mpinzani wa Ngoma afunguka Azam

Mshambuliaji mpya wa Azam, Ditram Nchimbi.

Muktasari:

  • Washambuliaji atakaowania nao namba kwenye kikosi cha kwanza ni mchezaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mwezi, Mei Shabani Idd, Yahya Zayd, Waziri Junior na Donald Ngoma ambaye amejiunga na Azam hivi karibuni kutoka Yanga.

Dar es Salaam. Mshambuliaji mpya wa Azam, Ditram Nchimbi amedai amejipanga vyema kukabiliana na kibarua cha kupata namba kwenye kikosi cha kwanza baada ya kujiunga na timu hiyo kutoka Njombe Mji.

Washambuliaji atakaowania nao namba kwenye kikosi cha kwanza ni mchezaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mwezi, Mei Shabani Idd, Yahya Zayd, Waziri Junior na Donald Ngoma ambaye amejiunga na Azam hivi karibuni kutoka Yanga.

Nchimbi amejiunga na Azam baada ya kutia saini mkataba wa miaka miwili ambao utamfanya kuitumikia klabu hiyo mpaka mwaka 2020.

Mshambuliaji huyo aliyeifungia mabao matatu Njombe Mji msimu uliopita, atakutana na changamoto ya kupigania namba kikosi cha kwanza na washambuliaji wengine watano.

Akizungumzia alivyojiandaa kukabiliana na changamoto hiyo, Nchimbi alisema atatumia vyema nafasi atakazopata kucheza ili kumshawishi kocha kumpa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

“Natambua kuwa hii ni klabu kubwa tofauti na Njombe Mji kwa hiyo hata malengo yake pia ni tofauti, kule tulikuwa tunapigania kutoshuka daraja, lakini huku ni ubingwa kwa hiyo nitajitahidi kuonyesha uwezo wangu wote ili kuisaidia Azam,” alisema Nchimbi.

Mshambuliaji huyo alisema hawezi kuchagua mchezaji wa kucheza naye katika kikosi cha kwanza Azam yenye maskani Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Hata hivyo, Nchimbi alishindwa kuinusuru Njombe Mji kushuka daraja.