Mourinho: Martial kaomba kuhama?

Tuesday May 15 2018

 

MANCHESTER, ENGLAND

JOSE Mourinho amesema hakuna ukweli wa kile kinachosemwa kuwa Anthony Martial amewasilisha mapendekezo ya kutaka kuhama Manchester United.

Baada ya Martial kukosekana kwenye mechi za hivi karibuni kumekuwa na uvumi kuwa Mfaransa huyo aliwasilisha barua ya kutaka kuachana na maisha ya Old Trafford ili akajaribu bahati yake kwingineko.

Staa huyo msimu huu amekuwa akisugua benchi baada ya Mourinho kushindwa kumtumia katika mechi mbalimbali.

Chelsea, Juventus, Bayern Munich na Olympique Lyon zote zimeonekana kuhitaji huduma ya mchezaji huyo ambaye alianzishwa kwenye mechi 18 tu za Ligi Kuu England.

Lakini, Kocha Mourinho alisema mchezaji huyo hakuwapo uwanjani kwa sababu anasumbuliwa na maumivu ya goti.

“Hayo ni mambo yenu tu, hayana ukweli. Ni majeruhi na anatibiwa goti,” alisema.

Mourinho anaamini Martial atakuwa fiti kwa ajili ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Chelsea wikiendi ijayo. Katika mechi hiyo, straika namba moja wa Man United, Romelu Lukaku anakimbizana na muda kupona enka aliyoumia dhidi ya Arsenal mwezi uliopita.