Moto wa Okwi, Bocco wamuibua straika Mbao

Muktasari:

  • Okwi raia wa Uganda, tayari amefunga mabao 19, huku Bocco akiweka kimiani mabao 14 na Obrey Chirwa wa Yanga akifuata kwa mabao 12.

STRAIKA wa Mbao FC, Rajeshi Kotecha amesema moto wa nyota wa Simba, Emanuel Okwi na John Bocco si wa mchezomchezo na hakuna wa kuuzima na mastaa hao wamempa somo kubwa.

Okwi raia wa Uganda, tayari amefunga mabao 19, huku Bocco akiweka kimiani mabao 14 na Obrey Chirwa wa Yanga akifuata kwa mabao 12.

Kotecha alisema kasi ya Okwi na Bocco si ya mchezo kwani wameonyesha uwezo wa hali ya juu pamoja na ukongwe wao lakini bado wako vizuri.

“Ni wachezaji wakongwe kwenye Ligi Kuu lakini wamekuwa wakijituma uwanjani hili ni somo kubwa kwetu sisi washambuliaji chipukizi, kikubwa ni kujituma kwenye mazoezi hadi uwanjani,” alisema Kotecha.

Straika huyo alisema mbali na wakali hao wa Simba, lakini pia kiungo, Pius Buswita wa Yanga naye anamuweka kwenye orodha ya wachezaji bora hadi sasa.

“Mtu asikudanganye, Okwi na Bocco ni habari nyingine, lakini kwa Yanga Buswita ndiye mkali na akiendelea hivi, atafika mbali kwa sababu ana uwezo,” alisema straika huyo.

Kinda huyo mwenye mabao mawili hadi sasa, alisema alitarajia kuwa miongoni mwa wachezaji wa kuwania kiatu cha mfungaji bora, lakini kutokana na kutocheza mechi nyingi amewaachia vita hiyo kwa wenye uwezo.

“Nimecheza mechi chache, kama nane hivi na nimefunga mabao mawili tu hadi sasa, lakini nilitamani sana kupambana kutwaa kiatu cha mfungaji bora, lakini naona nimeshakwama,” alisema.