Mo Salah kwa Messi chamtoto tu

Tuesday May 15 2018

 

LIVERPOOL, ENGLAND

MOHAMED Salah amevunja rekodi ya mabao kwenye Ligi Kuu England baada ya kutupia wavuni mara 32 katika mechi 38, lakini unaambiwa hivi mabao hayo ni chamtoto kwenye kushinda Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya.

Mabao hayo yanamfanya azidiwe kwa mabao mawili na Lionel Messi na staa huyo wa Barcelona bado ana mchezo mmoja umebaki, jambo linalomfanya kuwa na nafasi kubwa ya kuchukua tuzo hiyo ya ufungaji bora wa ligi zote za Ulaya.

Kwa sasa Messi ameshinda tuzo hiyo mara nne sawa na mpinzani wake wa karibu Cristiano Ronaldo na kwa hali ilivyo kwa sasa ataongeza tuzo ya tano labla kama kutatokea maajabu. Kwa sababu Salah ameshamaliza ligi, mchezaji pekee ambaye anaweza kumfanya Messi asibebe tuzo hiyo ni Ciro Immobile, ambaye pia amebakiza mechi moja huko kwenye Serie A, ambapo kikosi chake cha Lazio kitacheza na Inter Milan wikiendi ijayo. Staa huyo amefunga mabao 29, hivyo atahitaji kufunga mabao sita kumpiku Muargentina huyo.

Kama mabao yatabaki kuwa yalivyo, basi Harry Kane atakuwa amemaliza msimu kwenye nafasi ya tatu kutokana na kufunga mabao 30.