Mastaa sita watia presha makocha

Muktasari:

  • Kwa kitendo cha kupatikana bingwa tu, hiyo ina maana mashabiki kwa sasa wanasubiri kuona nani atakuwamo kwenye ile Top Four, huku wakisubiri kuona mipango ya msimu ujao kama kutakuwa na mabadiliko au Man City itaendeleza ubabe wake ikiwa chini ya kocha wake Pep Guardiola.

LONDON, ENGLAND

NDO hivyo, Ligi Kuu England inahesabu siku tu kabla haijatia nanga kusubiri msimu mwingine huku Manchester City tayari ikiwa imejibebea ubingwa wake.

Kwa kitendo cha kupatikana bingwa tu, hiyo ina maana mashabiki kwa sasa wanasubiri kuona nani atakuwamo kwenye ile Top Four, huku wakisubiri kuona mipango ya msimu ujao kama kutakuwa na mabadiliko au Man City itaendeleza ubabe wake ikiwa chini ya kocha wake Pep Guardiola.

Wakati ligi hiyo ikielekea kutia nanga, mashabiki wameshaanza mijadala ya mchezaji gani atasajiliwa na timu gani katika dirisha lijalo la usajili, huku kukiwa na mastaa kibao wa Ligi Kuu England, ambao wanaaminika huenda wasiendelee kubaki kwenye vikosi vyao baada ya msimu huu kukamilika.

Anthony Martial

(Man United)

Staa wa Ufaransa, Anthony Martial ameripotiwa kufikiria mpango wa kuihama Manchester United kwenye dirisha lijalo baada ya kuona Kocha Jose Mourinho hampi nafasi ya kutosha katika kikosi chake.

Mourinho amegoma kumpa Martial uhakika wa kucheza na hilo linamfanya staa huyo afikirie kuachana na maisha ya Old Trafford huku kuwa na ripoti Juventus inahitaji huduma yake. Ukweli Mourinho amekuwa na woga wa kumwaachia Martial kwa sababu anaogopa kisije kutokea kama kilichotokea kwa Kevin de Bruyne na Mohamed Salah alipowaachia huko Chelsea.

Mohamed Salah

(Liverpool)

Mo Salah alitua Liverpool mwaka jana tu hapo kwenye dirisha la majira ya kiangazi aliponaswa kutoka AS Roma kwa ada ya Pauni 35 milioni.

Lakini kiwango chake cha msimu huu hasa kwenye kutikisa mabao, kimemfanya staa huyo kuwindwa na timu kibao ikiwamo Real Madrid na Paris Saint-Germain, ambazo mwishoni mwa msimu zinaweza kutumia jeuri yao ya pesa kumng’oa staa huyo kutoka Anfield.

Huo ndiyo wasiwasi uliopo na kuna uwezekano Salah asiwepo kwenye kikosi cha Liverpool itakapofika msimu ujao kutokana na timu nyingi kupiga hesabu za kumsajili.

Riyad Mahrez

(Leicester City)

Kwenye dirisha la Januari alihusishwa na mpango wa kutimkia Manchester City kabla ya dili hilo kukwama na staa huyo kubaki Leicester City licha ya kusababisha matatizo makubwa. Lakini, Mahrez si kwamba anamvutia tu Kocha Pep Guardiola na kutaka amwongeze kwenye kikosi chake, staa huyo anawindwa na miamba wengine kibao ikiwamo Arsenal na Liverpool, hivyo kwa presha iliyopo, itakuwa bahati sana kwa Leicester City kama itaendelea kubaki na huduma ya winga huyo wa kimataifa wa Algeria baada ya msimu huu kumalizika. Mahrez anaendelea kuwa mchezaji bora kwa waliopo nje ya timu zilizopo kwenye Top Six.

Christian Eriksen (Tottenham)

Kumpoteza Eriksen hakika litakuwa pigo kubwa sana kwa Tottenham Hotspur hasa kutokana na ufundi wa kiungo huyo katika kutengeneza nafasi za mabao.

Staili yake ya kiuchezaji imeifungua macho Barcelona na hivyo inaamini ni mchezaji anayestahili kwenda kujiunga kwenye kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao baada ya kuona Ousmane Dembele akishindwa kuipa kile kilichokuwa ikikihitaji kukipata kutoka kwake.

Lakini, kupata huduma ya mchezaji kama Eriksen, basi itakulazimu kuwa na mkwanja unaoanzia Pauni 100 milioni na kuendelea kama lilivyo soko la wachezaji katika kipindi cha karibuni.

Kevin De Bruyne

(Man City)

Mashabiki wa Mancheester City hawatakuwa na chaguo jingine zaidi ya kuandamana tu wakati watakaposikia staa wao wa maana kwenye kikosi hicho, Kevin De Bruyne anaondoka. Huko nyuma, De Bruyne aliripotiwa kukubali kujiunga na Bayern Munich kabla ya kusajili dili jipya kwenye kikosi cha Man City.

Hata hivyo, jina lake bado linatajwatajwa huko Real Madrid na Barcelona na asikwambie mtu ni wachezaji wachache sana kwenye dunia hii ambao wataletewa ofa kutoka Barcelona au Real Madrid kisha wakagoma kwenda kujiunga nazo.

Matakwa yake ya kutaka kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na kutambulika kwenye tuzo za Ballon d’Or hilo ndilo litakalomfanya De Bruyne ang’oke Man City mwishoni mwa msimu huu kama kutakuwa na ofa ya kutoka Barca au Madrid.

David De Gea

(Man United)

Huwezi kuonekana kuwa ni waajabu kama utasema Manchester United isingekuwa na uhakika wa kuwamo kwenye Top Four ya msimu huu kama isingekuwa na huduma ya kipa David De Gea.

Hakika, De Gea ndiye mchezaji bora kabisa kwenye kikosi hicho cha Old Trafford na ndiyo maana wababe kama Real Madrid wamekuwa wakiifukuzia sana huduma yake.

Tangu Manuel Neuer alipoumia, De Gea anabaki kuwa kipa bora kabisa kwa sasa, akiwa na mechi kibao kwenye Ligi Kuu England alizocheza bila ya kuruhusu wavu wake kuguswa.

Haitashangaza kama kwenye dirisha lijalo De Gea ataachana na Man United na kwenda kujiunga na Los Blancos.

Mesut Ozil

(Arsenal)

Mjerumani, Ozil bado anabaki kuwagawa mashabiki wa soka kwenye Ligi Kuu England. Kundi linaloamini staa huyo ni matata, lakini kuna wengine wanaoamini mchezaji huyo ni bishoo, unamhitaji kwenye mechi nyepesi tu.

Hata hivyo, ukweli Ozil ni mchezaji wa kiwango cha juu sana na ndiyo maana Jose Mourinho alimtolea macho kwenye dirisha lililopita la Januari kabla ya mchezaji huyo kuongeza mkataba wake wa kuendelea kuitumikia Arsenal.

Ozil, ana ofa nyingine pia kutoka kwenye klabu za Ujerumani na kama Arsenal itashindwa kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, basi hilo linaweza kumfanya Mjerumani huyo akaamua kuondoka Emirates hata kama amesaini dili jipya miezi michache tu iliyopita.