Man City ilivyonasa pointi za ubingwa

Muktasari:

  • Ubingwa kapuni na bado kuna mechi tano mbele. Mechi 33, ushindi kwenye mechi 28, sare tatu na vichapo viwili tu.

MANCHESTERENGLAND

ASIKWAMBIE mtu, hakuna kitu kizuri kwa kipindi hiki kwa shabiki wa Ligi Kuu England kama kuishabikia Manchester City.

Ubingwa kapuni na bado kuna mechi tano mbele. Mechi 33, ushindi kwenye mechi 28, sare tatu na vichapo viwili tu.

Mabao 93 ya kufunga na 25 ya kufungwa, utasema nini tena kuhusu Man City wewe? Kuonyesha kuwa ubingwa wake ulikuwa wa hatari zaidi msimu huu, angalia msimamo wa ligi hiyo na uone pengo la pointi lililopo.

Hao Manchester United wanaoshika nafasi ya pili, wameachwa kwa pointi 16. Arsenal ndiyo kabisa imeachwa pointi 33, Chelsea imeachwa pointi 27, Liverpool ipo nyuma kwa pointi 17.

Yaani Top Six yote, hakuna hata timu moja iliyoweza kukimbizana na moto wa kikosi hicho cha kocha fundi wa mpira, Pep Guardiola.

Hivi ndivyo Man City ilivyogawa vipigo na kukusanya pointi zake ambazo zilitosha kuifanya inyakue ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Agosti 2017, pointi 7

Katika mwezi wa kwanza kabisa wa msimu huu wa Ligi Kuu England, Man City ilikusanya pointi saba kati ya tisa ilizopasa kunyakua katika mwezi huo wa Agosti, ambapo ilicheza mechi tatu, ikashinda mbili na kutoka sare mara moja.

Matokeo ya mwezi huo yalivyokuwa;

Bournemouth 1-2 Man City

Man City 1-1 Everton

Brighton 0-2 Man City

Septemba 2017, pointi 12

Kwenye mwezi wa pili wa msimu, gani la Guardiola lilianza kuchanganya na kushinda mechi zake zote nne ilizocheza Septemba, ikiwamo ushindi wa ugenini kwa Chelsea huko Stamford Bridge.

Kwa mwezi huo, Man City ilikusanya pointi zote 12 na hivyo kuifanya kuwa na pointi 17 katika msimamo wa ligi.

Matokeo ya mwezi huo yalivyokuwa;

Chelsea 0-1 Man City

Man City 5-0 Crystal

Watford 0-6 Man City

Man City 5-0 Liverpool

Oktoba 2017, pointi 9

Kwa mujibu wa Guardiola mwenyewe alianza kupata uhakika wa ubingwa wa msimu huu unaweza kuwa wake baada ya kupata ushindi kwenye uwanja mgumu wa Stamford Bridge. Baada ya hapo, kikosi chake kiliendelea kugawa dozi na kubeba pointi zote katika mechi zake ilizocheza Oktoba na kukifanya kuwa kwenye mwendo mzuri kabisa wa kuelekea kunyakua taji hilo.

Katika mwezi huo, Man City ilivuna pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu.

Matokeo ya mwezi huo yalivyokuwa;

West Brom 2-3 Man City

Man City 3-0 Burnley

Man City 7-2 Stoke

Novemba 2017, pointi 12

Katika mwezi huo, Man City ilikumbana na mmoja kati ya wapinzani wake kwenye Top Six na ikaonyesha imepania kufanya mambo makubwa kweli kweli msimu huu kwa kuangusha vichapo katika mechi zote nne ilizocheza Novemba.

Moja ya ushindi wake kwenye mwezi huo ni ule wa bao tatu dhidi ya Arsenal ambao ni moja ya wale waliopo kwenye Top Six na iliaminika ingesumbua katika msimu huu. Mwezi huo, Man City ilivuna pointi 12.

Matokeo ya mwezi huo yalivyokuwa;

Man City 2-1 S’ampton

Huddersfield 1-2 Man City

Leicester 0-2 Man City

Man City 3-1 Arsenal

Desemba 2017, pointi 19

Katika Ligi Kuu England, Desemba unatajwa kuwa mwezi mgumu zaidi na hapo ukiweka vizuri mipango yako, ndiyo mwezi wa kujihakikishia ubingwa kwenye ligi hiyo kwa sababu kuna mechi kibao zinazocheza katika mwezi huo.

Desemba hii, ilikuwa na mechi saba , ambazo ni sawa na pointi 21, lakini katika kuonyesha Guardiola ulikuwa msimu wake, alivuna pointi 19 na kupoteza mbili tu baada ya kushinda mechi sita na kutoka sare moja, nyumbani kwa Crystal Palace. Katika mwezi huu, Man City iliwachapa mahasimu wao, Man United Old Trafford.

Matokeo ya mwezi huo yalivyokubwa;

Crystal Palace 0-0 Man City

Newcastle 0-1 Man City

Man City 4-0 B’mouth

Man City 4-1 Tottenham

Swansea 0-4 Man City

Man Utd 1-2 Man City

Man City 2-1 West Ham

Januari 2018, pointi 9

Baada ya kutesa kwa mwaka wote wa 2017 tangu Ligi Kuu ilipoanza Agosti, Man City ilikwenda kukumbana na kipigo cha kwanza kwenye ligi hiyo, Januari mwaka huu, wakati ilipokwenda kuzabuliwa 4-3 ugenini huko Anfield, ilipomenyana na Liverpool.

Katika mwezi huo, Man City ilicheza mechi nne, ikachapwa moja na kushinda mechi tatu na hivyo kukusanya pointi ambazo zilizidi kuiweka kwenye nafasi nzuri ya kuelekea kwenye ubingwa wa ligi hiyo.

Matokeo ya mwezi huo yalivyokuwa;

Man City 3-0 West Brom

Man City 3-1 Newcastle

Liverpool 4-3 Man City

Man City 3-1 Watford

Februari 2018, pointi 4

Kasi ya Man City ilionekana kupunguza kwenye mwezi wa Februari baada ya kuonekana kuwa uchovu ulianza kuvamia kikosi hicho ambapo walicheza mechi mbili, wakashinda moja na kutoka sare nyingine. Kitu kiliachowashangaza wengi ni Man City ilitoka kuichapa bao tano Leicester City kisha ikaenda kutoka sare na Burnley, katika mechi ambayo chupuchupu wababe hao wa Etihad walikuwa wapoteze.

Matokeo ya mwezi huo yalivyokuwa;

Man City 5-1 Leicester

Burnley 1-1 Man City

Mach 2018, pointi 12

Baada ya kusuasua Februari, ilipofika Machi, Man City ilionekana kuja na nguvu kubwa na kushinda mechi zake zote nne ilizocheza kwenye mwezi huo, ikiwamo ya ushindi kwenye mechi mbili za vigogo wenzake wa Top Six, Chelsea na Arsenal. Uzuri kwa Man City ni kwamba kwenye mechi zote hizo mbili alicheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Etihad, akimchapa Arsenal Bao Tatu Bila na Chelsea aliishinda kwa bao 1-0. Lakini, yote kwa yote ni kukusanya pointi 12 za mwezi huo zilizowafanya kujihakikishia ubingwa bila ya mashaka yoyote.

Matokeo ya mwezi huo yalivyokuwa;

Everton 1-3 Man City

Stoke 0-2 Man City

Man City 1-0 Chelsea

Arsenal 0-3 Man City

Aprili 2018, pointi 3

Bado kuna mechi nyingine za kuchezwa kwenye mechi hii, lakini makala haya yanaandikwa, Man City ilikuwa imecheza mechi mbili kwenye mwezi huo, imechapwa moja na kushinda moja. Man City ilichapwa na mahasimu wao Man United huko Etihad, katika mechi ambayo kama wangeshinda tu wangetangaza ubingwa mapema kabisa, lakini kipigo cha 3-2 kilitibua hesabu zao. Baadaye, ilicheza na Tottenham huko Wembley na kushinda 3-1, matokeo ambayo yaliifanya kujiweka pazuri zaidi na kufanikiwa kutangaza ubingwa baada ya mahasimu wao Man United kuchapwa 1-0 na West Brom kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Matokeo ya mwezi huo yalivyokuwa;

Spurs 1-3 Man City

Man City 2-3 Man United.