Man City bingwa EPL, maswali yasiyojibika!

Muktasari:

  • Zikiwa zimesalia mechi chache, ni muhimu kutazama baadhi ya mambo, tukijiuliza na pengine kujibu tutakapoweza juu ya maswali husika ili kwa pamoja tuendelee na uchambuzi wa masuala haya ya soka, na ikiwezekana wadau wangu huko wayaliganishe na nchi walimo

LIGI Kuu ya England (EPL) ndiyo inafuatiliwa kwa karibu na watu wengi zaidi duniani – ndiyo maarufu zaidi na sasa inaelekea ukingoni, ambapo watu watakosa uhondo, lakini kwa mwaka huu watajielekeza kwenye fainali za Kombe la Dunia.

Zikiwa zimesalia mechi chache, ni muhimu kutazama baadhi ya mambo, tukijiuliza na pengine kujibu tutakapoweza juu ya maswali husika ili kwa pamoja tuendelee na uchambuzi wa masuala haya ya soka, na ikiwezekana wadau wangu huko wayaliganishe na nchi walimo:-

Je, Man City wanaweza kuvunja rekodi ya pointi?

Tayari Manchester City imechukua ubingwa kwa kufikisha pointi 87 huku ikibakiwa na mechi tano mkononi. Watahitaji kushinda mechi nne ili kuvunja rekodi iliyowekwa na Chelsea msimu wa 2004/5 walipopata ubingwa wa kwanza na ujio wa Jose Mourinho kama kocha wao. Kimsingi wanaweza, japokuwa hapa nyuma waliteleza na kuchezea vichapo ndani na nje ya EPL. Wakitia kasi sana watafikisha alama 100. Itategemea iwapo watarudi kwenye mserereko wao wa ushindi au labda wakitwaa ubingwa watazima gesi inayotoa moto wao mkali.

Je, MOURINHO aTaondoa utata juu ya muhula wake Man United?

Mashabiki wa United wangependa kumwona Mourinho akibaki, lakini hadi sasa hakuna uhakika kwamba atabaki maana kuna wakati hatabiriki. Aliongeza mkataba wake mapema mwaka huu lakini baada ya hapo akaanza kuonesha zile dalili zake za kutoridhishwa na baadhi ya vitu, ikiwamo ugomvi na wachezaji kadhaa. Pengine kufanikiwa kuwafunga Man City, tena Paul Pogba aliyekuwa akimtupa benchi akiwa ndiyo injini, kutamaliza matatizo ndani mwake.

Lakini bado; amekuwa akilalamika kwamba City wamewaacha mbali mno na anahitaji kusajili wachezaji wa kiwango cha juu; waliondoshwa mapema kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) na Sevilla katika hali ya aibu na kushangaza na haitasahaulika kirahisi, labda kwa vile na City walitolewa kwa fedheha zaidi na Liverpool. Nionavyo ni kwamba, akiweza kukusanya ushindi zaidi katika EPL, akatwaa Kombe la FA, atakuwa na raha na salama na atabaki. Anacheza na Chelsea Jumamosi ijayo kwenye nusu fainali ya Kombe la FA wakati nusu fainali nyingine ni Tottenham Hotspur na Southampton.

Je, Liverpool wanaweza kumaliza ligi wakiwa bora kuliko 19 waliobaki?

Vijana wa Jurgen Klopp wamekua, wana kasi na kiwango cha aina yake hivyo kwamba sasa ni tishio kwa timu nyingi wakiwa na Mo Salah. Waliwakung’uta Manchester City bila huruma nyumbani na ugenini. Wamekuwa wazuri na sasa wanaonesha kwamba ukiachilia Manchester City kwa msimu huu, wanaweza kuwa bora kuliko hao 19 waliobaki. Wakiziba mapengo hapa na pale, Liverpool watakuwa washindani wa karibu sana wa City msimu ujao, wakibaki na Salah, naye aendelee na kiwango chake, si kama Leicester na watu wake baada ya kutwaa ule ubingwa.

Je, Chelsea wataweza kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya?

Chelsea wamekuwa na msimu mbaya au mgumu kuendana na jinsi mmoja atakavyoamua neno la kutumia. Walishachakazwa 2-0 na Southampton hadi saa nzima ilipokamilika Jumamosi iliyopita, lakini Olivier Giroud aliyetoka Arsenal akatia mawili na Eden Hazard moja na kuchomoa, walau kumtunzia heshima kocha Antonio Conte anayesemwa kwamba ataondoka mwisho wa msimu.

Hawa ni mabingwa watetezi lakini wanakwenda ndivyo sivyo, wakiwa alama 10 nyuma ya wale wanaoshika nafasi ya nne, inamaanisha kwamba itakuwa ngumu kufuzu, hivyo wakicheza huenda wakaangukia Ligi ya Europa waliko Arsenal msimu huu. Conte amekuwa akilalamikia uhaba wa wachezaji pia – washambuliaji wake ni butu, wakati huu ambapo mmiliki, Roman Abramovich anaonekana kutokuwa na nia ya kumwaga fedha nyingi kwa ajili ya usajili. Si rahisi kwa Liverpool na Spurs wawaachie katika nafasi mbili za mwisho kwenye nne bora, hivyo ni vyema wakajiandaa tu kusaikolojia kumaliza wakiwa nafasi ya tano au ya sita.

Je, kiatu cha dhahabu kitaenda kwa nani? Salah au Kane

Alipokata rufaa kulalamika kwa Christian Eriksen kupewa bao lililofungwa dhidi ya Stoke na kulipewa ili afikishe mabao 25 dhidi ya 29 ya Mo Salah wa Lverpool, Harry Kane alishambuliwa sana kwenye mitandao ya jamii hadi akaonesha kuumizwa sana, na kocha wa Spurs, Mauricio Pochettino akasema mchezaji wake huyo anaumia sana.

Salah alimbeza mtandaoni pia kwa kugombea bao ambalo EPL walikuwa wamempa Eriksen kwa sababu mpira ule wa kasi ulimgusa kwa mbali wala ikiwa hangeugusa hapangekuwapo mabadiliko ya hali ya bao. Je, Kane atafanikiwa kumpita Salah na Sergio Aguero ataweza kutoka huko kwenye mabao 21 aliyokuwa nayo Aprili 14 na kupanda zaidi kuwapita? Nionavyo Salah hatasimamishwa na mtu labda aumie, japokuwa ukweli ni kwamba mpira unadunda – ni mmoja kati ya watatu hawa.

Je, Burnley watamaliza ligi juu ya Arsenal?

Arsenal wamekuwa kwenye nafasi ya sita kwa muda sasa, bila kujali wao wanashinda au walio juu yao wanafanyaje, na hiyo ni kuonesha jinsi gani msimu huu na uliopita vijana wa Arsene Wenger wamekuwa na wakati mgumu, licha ya kwamba wamefanya vyema kwenye njia nyingine – Ligi ya Europa. Wakifanikiwa kuwapiga Atletico Madrid kwenye nusu fainali, labda watatwaa ubingwa na kuingia UCL kwa njia aliyotumia Mourinho msimu jana.

Lakini nyuma yao wapo Burnley wanaoonekana kuwa wazuri kadiri muda unavyokwenda. Awali Arsenal na washabiki wake walikuwa wakihakikisha wanamaliza ligi juu ya mahasimu wao wa London Kaskazini – Spurs, lakini leo Arsenal wametupwa chini kabisa, labda wajirekebishe msimu ujao. Sasa kuna tishio jingine – Burnley wanataka wamalize juu yao. Kocha Sean Dyche anajituma na amefikia hata kufikiriwa kuchukuliwa na klabu kubwa, kama si Arsenal hao hao kuwabadili wakongwe wanaoonekana kuishiwa mbinu.

Je, Allardyce anastahili msimu mzima klabuni Everton?

Washabiki wa soka ni watu wa ajabu; wakati mwingine hata viongozi. Everton walikuwa katika hatari ya kushuka daraja, wakamchukua Big Sam, au Sam Allrdyce ambaye ni mtaalamu wa kuziondoa timu huko kama alivyofanya kwa Sunderland na Crystal Palace. Kazi hiyo kwa Everton aliikamilisha siku zake chache za mwanzo, lakini labda aliitwa mapema mno, kwani baada ya hapo ni kana kwamba ameweka breki ya mkono – Everton hawaendi tena kwa kasi huko juu; ni kamavile hawakutaka ubingwa wala kucheza michuano ya Ulaya. Washabiki hawamtaki, wanasema kwanza mfumo wake unachusha. Je, atapewa msimu mzima tena au ataondoshwa ili aitwe dakika za mwisho kunusuru ikiwa tatizo litawakumba? Tusubiri tuone.

Je, Timu zilizoshuka daraja zitabaki zote juu?

Wakati West Bromwich Albion wanaonekana kwamba kikombe chao kimejaa na wanaondoka EPL kushuka, Stoke wanang’ang’ana kidogo na Southampton wanaonekana bado limewaganda. Laiti wangeshikilia bao zao mbili dhidi ya Chelsea na kuwazuia kufunga, walau wangeepuka, sasa kazi ngumu ipo. Juu yao wapo Crystal Palace ambao bosi wa zamani wa Timu ya Taifa ya England, Roy Hodgson anasema ni tatizo la kisaikolojia tu; wanaweza kuchomoa. Kuna uwezekano kwamba timu zote zilizopanda daraja msimu huu zikabaki juu – Brighton, Newcastle na Huddersfield. Brighton wanaofundishwa na mweusi pekee EPL, Chris Hughton hata waliwafunga Arsenal . Rafa Benitez anawaongoza vyema Newcastle wakati David Wagner anagangamala na Huddersfield wenye umoja wa aina yake.