‘Malkia wa Soul’ Aretha Franklin amefariki dunia leo

Detroit, Marekani. Gwiji wa muziki wa soul,Aretha Franklin amefariki dunia leo akiwa na umri wa miaka 76.

Aretha Franklin "queen of soul" alitamba na nyimbo zake  Respect na Think amefariki akiwa nyumbani kwake Detroit.

Malkia huyo wa muziki wa Soul alikuwa akisumbuliwa na saratani tangu 2010 na mwaka jana alitangaza kustaafu muziki.

Franklin alikuwa na nyimbo zaidi ya 20 zilizoshika namba mmoja katika chati ya muziki Marekani kwa miongo saba ya uhai wake.

Mwaka jana Novemba alifanya tamasha lake la mwisho jijini New York kwa kusaidiana na Elton John Aids Foundation.

Katika taarifa iliyotolewa na familia yake ilisema: "Ni moja ya siku ngumu kwetu tumeshindwa hata kuwa na maneno mazuri ya kuzungumzia huzuni yetu.

"Tumepoteza nguzo ya familia yetu. Mapenzi yake aliyokuwa nayo kwa watoto wake, wajukuu, vitukuu na vilembwe vyake hauna mfano."

Katika miaka yake sabini ya uimbaji, Franklin alijijenga na kuwa mmoja ya wanamuziki wa kipekee katika tasnia hiyo, alifanikiwa kushinda tuzo 18 Grammy Awards, akiwa ameuza zaidi ya nakala 75 milioni za nyimbo zake duniani.

Alikuwa mwanamke wa kwanza kutumbuiza katika tamasha la Rock and Roll Hall of Fame, pia anarekodi ya kuingiza nyimbo 112 katika charti za Billboard, hiyo imemfanya kuwa mwanamke mwenye mafanikio zaidi katika historia ya mauzo.

Franklin pia alipata tuzo nyingine katika maisha yake ya muziki akiwa ametwaa tuzo tatu za American Music Awards, mbili za MTV Video Music Awards, tatu NAACP Image Awards, mmoja ya Golden Globe, na Presidential Medal of Freedom, pamoja na Hollywood Walk of Fame, Grammy Legend Award na Grammy Lifetime

Franklin alizaliwa Memphis Machi 25, 1942. Familia yake ilihamia Detroit akiwa na miaka 5, na mama yake Barbara alifariki kabla ya Franklin kufikisha umri wa miaka 10.

Baba yake Clarence LaVaughn “C. L.” Franklin, alikuwa mchungaji mashuhuri Detroit’s New Bethel Baptist Church, na nyumbani kwao walikuwa wakitembelewa na watu mashuhuri kama Martin Luther King Jr., Jackie Wilson, Sam Cooke, na Mahalia Jackson.

Baada ya kifo cha mama yake Aretha alilelewa na marafiki hao wa baba yake ambako alipata nafasi ya kujifunza muziki na kupiga kinanda katika kanisa la baba yake New Bethel.

Franklin ni mama wa watoto wawili ambao aliwapata akiwa na umri wa miaka 14, mtoto wake wa kwanza, Clarence alijifungua akiwa na umri wa miaka 12,  na mtoto wa pili Edward, alijifungua miaka miwili baadaye. Baadaye alibarikiwa kupata watoto wawili wengine wa kiume, Teddy Richards na Kecalf Cunningham katika mwaka 1964 na 1970.).

Hata hivyo, pamoja na kuanza maisha ya ulezi mapema havikumzuia Franklin kuendeleza ndoto yake ya uimbaji wa nyimbo za injili akiwa na miaka 14.

Akiwa chini ya usimamizi wa baba yake alisaini mkataba na J.V.B. Records, alitoa albumu yake ya kwanza, Songs of Faith, mwaka 1956. Wakati alipotimiza miaka 18, aliamia katika muziki kidunia baada ya kuingia mkataba wa kurekodi na Columbia Records.