Liverpool, Real Madrid zatajwa ubingwa Ulaya

Muktasari:

  • Keane aliyewahi kuwa Manchester United na Dixon, aliyekuwa beki wa Arsenal wametofautiana kwenye utabiri wao huku mmoja akichagua Liverpool na mwingine Real Madrid.

LONDONENGLAND


MAGWIJI wa klabu za Ligi Kuu England, Roy Keane na Lee Dixon wametoa utabiri wao wa timu ambayo wanadhani itashinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Keane aliyewahi kuwa Manchester United na Dixon, aliyekuwa beki wa Arsenal wametofautiana kwenye utabiri wao huku mmoja akichagua Liverpool na mwingine Real Madrid.

Timu zilizoingia nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ni AS Roma, Liverpool, Real Madrid na Bayern Munich, lakini wakali hao wa zamani kwenye soka la England wanaamini Los Blancos na wababe wa Anfield mmoja wapo ndiye atakayeibuka na ubingwa wa michuano hiyo ambapo fainali yake itapigwa huko Kiev. Dixon anaamini Liverpool ndio itabeba ubingwa, akisema: “Liverpool ina nafasi kubwa kutokana na wale mafowadi wake watatu. Hata kama watapangwa na Real Madrid na wale mabeki wao wa hovyo wa pembeni, nadhani Liverpool ina uwezo wa kumchapa yoyote yule.”

Keane anaipa nafasi Real Madrid na kusema sababu ya kufanya hivyo ni kuwapo kwa Cristiano Ronaldo.

“Sawa wana kipa wa hovyo, wana makosa mengi kwenye beki, lakini kwenye mechi hizo zijazo Ramos atakuwa amerudi. Real Madrid ina nafasi kutokana na uzoefu wa Ronaldo, ambaye ndiye mtu wake inayemtegemea.” Keane pia amedai kuongezeka kwa Virgil van Dijk kumeifanya Liverpool kuanza kuwa na uimara kwenye beki yake.