Liverpool, PSG waiteka Ulaya

Muktasari:

  • Timu hizo mbili msimu uliopita ziliweka rekodi ya kufunga mabao mengi katika mechi za hatua ya makundi

London, England. Vumbi la Ligi ya Mabingwa Ulaya litatimka leo kwenye viwanja mbalimbali barani humo ingawa macho zaidi ni mchezo kati ya Liverpool na Paris Saint-Germain ya Ufaransa utakaopigwa saa 3:45 usiku.

Mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Anfield mjini Liverpool, ndio umekuwa gumzo kila kona na  mvuto wa mchezo huo unatokana na ubora na umahiri wa safu za ushambuliaji za timu hizo.

Rekodi

Liverpool inaingia kwenye mchezo huo ikitoka kushinda mechi tano mfululizo za Ligi Kuu England msimu huu, ikiwa ni mara ya kwanza kwao tangu msimu wa mwaka 1990/91.

Kocha wa timu hiyo Jurgen Klopp, ameapa kuendeleza wimbi hilo la ushindi pamoja na nia ya kuweka rekodi dhidi ya PSG kwani kabla ya mchezo wa leo timu hizo zimekutana mara mbili pekee kila moja ilishinda mchezo wa nyumbani.

Timu hizo zilikutana kwa mara ya kwanza katika nusu fainali ya Kombe la Washindi Barani Ulaya, Aprili 10, 1997, PSG ikiwa mwenyeji iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Liverpool.

Katika mchezo wa pili wa nusu fainali wakiwa nyumbani Liverpool waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 mchezo uliopigwa Aprili 24, 1997 hivyo kung’olewa kwa tofauti ya bao moja.

Hii ni mara ya kwanza kwa Liverpool kucheza na PSG katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na zinakutakana huku zikiwa na vikosi vinavyofanana zote zikijivunia zaidi makali ya safu za ushambuliaji.

Kama ilivyo kwa PSG Liverpool safu ya ushamuliaji ya Liverpool inatikisa katika Ligi Kuu England, imeiwezesha kushinda mechi zote inajivunia zaidi ubora wa Mohamed ‘Mo’ Salah, Roberto Firmino na Sadio Mane, wanaopikiwa mipira na Naby Keita, Fabinho, Georginio Wijnaldum, James Milner, Jordan Henderson na Adam Lallana, kwa ujumla wamefunga mabao 11 katika mechi tano za ligi kuu.

Katika ulinzi imeimarika zaidi baada ya kumsajili kipa wa kibrazil, Alisson anayempa changamoto aliyekuwa kipa namba Simon Mignolet, wanaohakikishiwa usalama na ulinzi wa Virgil Van Dijk, Dejan Lovren, Joel Matip, Andrew Robertson, Nathaniel Clyne na Alberto Moreno, safu hiyo ya ulinzi imeruhusu mabao mawili tu katika ligi kuu hadi sasa.

Kwa upande wao PSG pia safu yao ya ushambuliaji inayoongozwa na mkongwe Edinson Cavani, Neymar, Angel Di María, Kylian Mbappe, Eric Maxim Choupo-Moting, Timothy Weah na Moussa Diaby.

Washambuliaji hao kwa ujumla wao wameiweka PSG kileleni wa Ligue 1 kwa mabao yao 17 katika mechi tano za mwanzo za Ligi Kuu Ufaransa, huku safu ya ulinzi inayoongozwa na kipa mkongwe wa Italia, Gianluigi Buffon akisaidiana na Alphonse Areola imeendelea kuwa kizingiti cha aina yake.

Mbali ya mtanange huo, leo pia zitapigwa mechi kibao za michuano hiyo Inter Milan itaikaribisha Tottenham Hotspur, Barcelona dhidi ya PSV, Schalke 04 vs Porto, Monaco vs Atletico Madrid, Crvena Zvezda vs Napoli, Galatasaray vs Lokomotiv Moskva na Club Brugge vs Borussia Dortmund.