Kumbe Mourinho alimtaka Kante bana!

N’Golo Kante.

Muktasari:

Mwanasoka huyo ghali pale Manchester United baadaye alisema kuwa kucheza kwake kwa kiwango bora kile kulitokana na kwamba kwenye kikosi alikuwapo mtu anayeitwa N’Golo Kante ambaye alifanya kazi zote za kukaba na yeye akabaki na jambo moja tu, kucheza kwa uhuru.

MANCHESTER, ENGLAND. SI uliuona ule mpira mwingi alioupiga, Paul Pogba, kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizotimka kule Russia akiwa na Ufaransa?

Mwanasoka huyo ghali pale Manchester United baadaye alisema kuwa kucheza kwake kwa kiwango bora kile kulitokana na kwamba kwenye kikosi alikuwapo mtu anayeitwa N’Golo Kante ambaye alifanya kazi zote za kukaba na yeye akabaki na jambo moja tu, kucheza kwa uhuru.

Basi bana, kusikia hivyo, kocha Jose Mourinho, akafanya mpango wa chini kwa chini kumnasa mkata umeme huyo wa Stamford Bridge, Kante, ili atue kwenye kikosi chake katika usajili wa majira ya kiangazi ambao dirisha lake lilifungwa jana Alhamisi.

Mourinho alipanga kufanya uvamizi mwingine huko Chelsea kwa msimu wa pili mfululizo baada ya mwaka jana kwenye uhamisho wa majira ya kiangazi kutua kwenye timu hiyo kumnyakua Nemanja Matic.

Wakati mpango wa kumsajili Willian ukiwekwa wazi, lakini huu wa Kante ulikuwa wa kimyakimya.

Wakala wa kiungo wa Kibelgiji, Axel Witsel, ndiye aliyefichua jambo hilo baada ya kuwapo kwa taarifa kwamba mteja wake alikataa ofa ya kutua Old Trafford na kwenda kujiunga na Borussia Dortmund.

Wakala huyo, Paul Stefani, alisema Mourinho hakumtaka Witsel na akili yake ilikuwa kwa Kante. Mwaka jana, Mourinho alimnasa Matic kwa ada ya Pauni 40 milioni.

Stefani alisema: “Nina taarifa za uhakika kabisa Mourinho alisema anamtaka Witsel, lakini halikuwa chaguo lake la kwanza. N’Golo Kante ndiye aliyekuwa akishika namba moja kwenye machaguo yake.”

Mourinho, leo Ijumaa anatarajia kuiongoza Man United katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu England dhidi ya Leicester City utakaopigwa Old Trafford huku kikosi chake kikikabiliwa na majeruhi kibao kuanzia Matic, Ander Herrera, Marcos Rojo, Antonio Valencia na wengineo.