Kocha Mbelgiji aipania Simba Day

Muktasari:

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini leo, Aussems alisema mechi hiyo imekuja wakati muafaka kwa Simba kupima ufanisi wa kambi yao ya wiki mbili nchini Uturuki.

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Patrick Aussems amesifu uongozi wa timu hiyo kwa kuileta nchini Asante Kotoko ya Ghana kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya timu yake kesho kwenye tamasha la Simba Day.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini leo, Aussems alisema mechi hiyo imekuja wakati muafaka kwa Simba kupima ufanisi wa kambi yao ya wiki mbili nchini Uturuki.
"Kwangu mimi naichukulia mechi hii zaidi ya kuwa ya kirafiki bali kama fursa ya muendelezo wa maandalizi kwa timu yangu kuelekea mashindano ya kimataifa mwakani.
Kotoko ni timu kubwa na naamini watakuwa kipimo bora kwetu hivyo nawaomba wapenzi, mashabiki na wanachama wa Simba kujitokeza kwa wingi kuona nini tumekifanya Uturuki," alisema Aussems.

Kocha wa Kotoko, Fabian Samuel alisema wanaamini mchezo dhidi ya Simba utakuwa na hamasa na msisimko wa kipekee.
"Kwa sasa ligi ya kule kwetu imesimama hivyo tunawashukuru Simba kwa kutualika kwa sababu inatupa nafasi ya kutuweka fiti," alisema Samuel.