Kocha Mbao asitisha bata kwa wachezaji wake

Muktasari:

Mbao katika msimu wake wa kwanza katika Ligi Kuu iliweka rekodi ya kucheza fainali ya Kombe la FA

Mwanza. Mambo magumu, benchi la ufundi la klabu ya Mbao FC limesema ili kuhakikisha timu hiyo inabaki Ligi Kuu msimu ujao,hakuna mchezaji yeyote kwenda likizo badala yake ni mazoezi mwanzo mwisho.

Hadi sasa Mbao imevuna pointi 19 na kukaa nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, inahitaji ushindi zaidi katika mechi zilizobaki ili kunusurika na janga la kushuka daraja.

 Kocha Msaidizi wa kikosi hicho, Ahmad Ally alisema wameazimia kuendelea na mazoezi kuhakikisha ligi itakapoendelea waweze kupata matokeo mazuri.

 Alisema kiufundi wamebaini umakini kwa vijana wao ndio tatizo haswa eneo la ushambuliaji ambalo linashindwa kufunga mabao ya wazi na kwamba watajipanga kurekebisha mapungufu hayo.

 “Sisi tunaendelea na mazoezi kwa sababu tukisema kupumzika vijana wanajisahau na ukiangalia msimamo hatupo salama, hivyo tumeazimia kujifua zaidi ili kupata matokeo mazuri,” alisema Ally.

 Kocha huyo aliongeza kuwa mazoezi watakayodili nayo haswa kipindi hiki ambacho Ligi imesimama ni kuwajenga nguvu kwa wachezaji ili kukomaa zaidi.

Alisema Ligi imekuwa ngumu kwani kupoteza mechi sita mfululizo ugenini iliwatibulia mipango yao na kwamba hapa wanaelekeza nguvu katika mechi zijazo.

 “Kwa ujumla ligi imekuwa ngumu na ushindani mkali, zile mechi za ugenini sita tulizopoteza mfululizo zilituharibia mipango yetu, ila tunajipanga upya”alisema Ally.