Kocha Barcelona amfuata Wenger

Muktasari:

  • Valverde analazimika kuachia ngazi licha ya kuipa mataji mawili katika msimu mmoja aliyodumu Barcelona.

London, England.Kocha wa Barcelona Ernesto Valverde anatarajiwa kuondoka mwishoni mwa msimu huu.

Valverde analazimika kuachia ngazi licha ya kuipa mataji mawili katika msimu mmoja aliyodumu Barcelona.

Kauli ya Valverde imekuja siku chache baada ya kocha mwingine nguli duniani Arsene Wenger kutangaza kuachia ngazi mwishoni mwa msimu huu.

Kocha huyo mwenye miaka 54, ameipa Barcelona Kombe la Mfalme na anajiandaa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Hispania msimu huu.

Valverde ameingia matatani baada ya Barcelona kutupwa nje katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufungwa na AS Roma.

Chanzo cha ndani kimedai kocha huyo amechukizwa na lawama anazopata kutoka kwa maofisa wa Barcelona.

Muda mfupi baada ya kuondolewa kwenye mashindano hayo, maofisa wa klabu hiyo ya Nou Camp walianza mkakati wa kusaka kocha mpya majira ya kiangazi.

Licha ya kutwishwa mzigo wa lawama, wachezaji wanataka kocha huyo kuendelea na kibarua.

Tangu mwaka 2008 Barcelona imebadilisha makocha watano tofauti Pep Guardiola, Tito Vilanova, Gerardo Martina, Luis Enrique na Valverde.