MAONI YA MHARIRI: Klabu kubwa zisipewe nafasi ya kuua vipaji vya chipukizi wetu

Muktasari:

Bahati mbaya ni klabu chache zinazotekeleza jambo hilo kwa ufanisi, kiasi unaweza hata kuzihesabu.

KWA muda mrefu wadau wa soka nchini kuanzia viongozi wa FA ngazi za wilaya mpaka taifa na hata wale wa klabu na wanahabari wamekuwa wakiimba wimbo moja.

Wimbo wa kutaka kuwepo kwa uwekezaji katika soka la vijana kwa kuamini kuwa ndio msingi wa mafanikio ya kandanda letu. Ndio maana kila mara tumekuwa tukisikia zikitolewa maagizo kwa klabu kutoka FA juu ya kutakiwa kuwa na timu za vijana, huku ikianzishwa miradi na michuano mbalimbali ya vijana.

Bahati mbaya ni klabu chache zinazotekeleza jambo hilo kwa ufanisi, kiasi unaweza hata kuzihesabu.

Hata kwenye madirisha ya usajili kumekuwa na ngonjera za klabu kusajili wachezaji vijana kwa nia ya kutaka kuwajengea misingi mizuri ya soka kwa manufaa ya taifa mbele ya safari.

Lakini ukifuatilia ni maigizo matupu katika mikakati na mipango hiyo inayotangazwa na sajili zinazofanywa na klabu. Turejee kwa sasa wakati dirisha dogo la usajili likiendelea kuwa wazi na hata katika usajili wa dirisha kubwa uliofanyika mwanzoni mwa msimu huu.

Klabu nyingi bado zimekuwa zikifanya usajili kishabiki zaidi na kutafuta sifa, huku zikizidi kuonyesha namna gani zisivyothamini na kuwaamini vijana wanaowasajili ama kuwa nao kwenye vikosi vyao na kuendelea kuendeshwa na mhemko tu. Klabu zimekuwa zikisajili wachezaji vijana kwa fujo, lakini wakishindwa kuwapa nafasi za kuzitumikia timu hizo, kitu kinachokatisha tamaa na kuua vipaji vyao.

Klabu kubwa zimekuwa mahandaki la kuua vipaji vya vijana kwa kupenda kuwarundika pamoja na kushindwa kuwatumia kabla ya kuwaacha wakiwa wamechanganyikiwa.

Rejea kwenye mfano halisi wa Kipa Manyika Peter, kijana huyu alikuwa Simba pamoja na Dennis Richard, lakini hawakupewa nafasi ya kucheza kwa vile kikosini kulikuwa na makipa wageni.

Wachezaji hao wameachwa na wengine kutolewa kwa mkopo, lakini huko walipo kwa sasa wanafanya vizuri. Manyika akiwa kipa tegemeo wa Stand United kiasi cha kushangaza.

Azam ni moja ya klabu ya kutolewa mfano kwa kuthamini soka la vijana na kuwapa nafasi wachezaji wao, kwa mfano misimu kadhaa nyuma walikuwa na Mwadini Ali, lakini waliamua kumpa nafasi Aishi Manula. Leo utazungumza nini kuhusu Manula, kipa huyo amekuwa mmoja ya makipa bora kabisa nchini kwa sasa. Yanga ilivutiwa na kipa wa Serengeti Boys, Ramadhani Kabwili na kumsajili, lakini imemtumia katika mechi ngapi?

Huku ni kuviza vipaji vya wachezaji wetu vijana, ni sawa tu na anachofanyiwa Jamal Mwambeleko na wengine waliosajili kwa mbwembwe na klabu hizo kubwa wakitokea timu za mikoani kisha kukalishwa benchi na kuwa wachezaji waa majukwaani. Hii sio sawa na Mwanaspoti inakemea mtindo huu wa kuviza vipaji vya wachezaji unaofanywa na klabu kubwa. Yanga imekuwa ikipigiwa kelele kuwa ina tatizo la kiungo mkabaji, ila kikosini ina kina Said Juma ‘Makapu’ na Pato Ngonyani, vijana kabisa, lakini wamekuwa wakichezeshwa kwa machale. Hawapewi nafasi, yaani hawaminiwi.

Klabu zetu zimekuwa zikitumia fedha nyingi kusajili wachezaji wa kigeni hata katika nafasi zisizohitaji wachezaji wa aina hiyo, hili linapaswa kubadilishwa. Wageni na wazoefu ni muhimu vikosini, lakini tuwaamini vijana tunaowasajili kwa manufaa ya taifa.

Pia, klabu ziache kufanya usajili wa sifa na kutaka kuwafurahisha mashabiki, badala yake waangalie uhalisia wa soka letu na maendeleo yake. Ndio maana kila msimu zinanyakua kila wachezaji waliovuma na kuwasumbua, kisha kuwajaza vikosini mwao bila kuwatumia na kusababisha kuua vipaji vyao.

Imefika wakati viongozi wa klabu na wadau wake wakabadili mfumo wa kuishi kwa mazoea na kufanya mambo kwa maendeleo ya soka la klabu zao na Tanzania kwa jumla. Tunaachwa mbali na majirani zetu kwa mtindo huu wa mihemko kila uchao na kupuuza nguvu kazi ya vipaji vya vijana.

Tusiwakatishe tamaa na kuua vipaji vyao kwani kufanya hivyo ni kulididimiza soka la Tanzania. Tunahaha kusaka timu kali ya taifa, kwa sasa hatuwajali na kuwathamini vijana wetu kwa kuwapa nafasi badala yake tunaviza vipaji vyao. Tuacheni mtindo huu kwa kuwa hauna faida kwetu!