Kinda la Arsenal lawika Ujerumani

Muktasari:

  • Katika muendelezo wa Ligi Kuu Ujerumani,  mkongwe Arjen Robben alifunga bao maridadi kuipa Bayern Munich ushindi wa 3-1 dhidi ya Bayer Leverkusen

Munich, Ujerumani. Mshambuliaji kinda wa Arsenal, Reiss Nelson, anayekipiga kwa mkopo katika timu ya Hoffenheim ya Ligi Kuu Ujerumani ameendelea kufanya mambo makubwa uwanjani.

Kinda huyo mwenye miaka 19, ambaye anacheza kwa mara ya kwanza katika Bundesliga, juzi Ijumaa alifunga bao la kusawazisha kwa timu yake ilipocheza na Fortuna Dusseldorf, ingawa mchezo ulimalizika kwa kichapo cha mabao 2-1.

Mchezaji huyo alikuwa akifunga mabao katika mechi kadhaa za kirafiki na hakuna aliyekuwa akimpa nafasi ya kung’ara pale ligi itakapoanza lakini kwa sasa amekuwa na mchango mkubwa kwenye timu.

Alikaribia kuipa timu yake pointi moja kama si mchezaji mwingine anayecheza kwa mkopo kutoka Watford, Dodi Lukebakio kuifungia Fortuna Dusseldorf, bao la ushindi kwa njia ya mkwaju wa penalti dakika mbili kabla ya kipenga cha mwisho.

Nelson na Dodi ni muendelezo wa makinda wa England kutamba katika Ligi Kuu Ujerumani kwani chipukizi mwingine Jadon Sancho mwenye miaka 18, alitengeneza mabao mawili kuiwezesha Borussia Dortmund kuichapa Eintracht Frankfurt kwa mabao 3-1.