Kaka astaafu soka

Muktasari:

  • Kaka ametwaa taji tuzo mwanasoka bora wa dunia wa mwaka 2008, pia ametwaa taji la Ligi ya Mabingwa akiwa na AC Milan

Mchezaji nyota wa zamani wa AC Milan, Ricard Kaka ametangaza kustaafu soka baada ya kucheza kwa mafanikio.

Kaka amestaafu soka juzi usiku huku timu yake Orlando City ikilala bao 1-0 ilipovaana na Columbus katika mchezo wa Ligi Kuu Marekani.

Hata hivyo, mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil, alishindwa kujizuia kububujikwa machozi wakati akiaga mashabiki uwanjani.

Mchezaji wa Columbus Ola Kamara alifunga bao pekee katika mchezo huo ambao Orland City ilikuwa nyumbani.

Kaka amestaafu soka akiwa mmoja wa wachezaji nyota waliotamba Ulaya. Kiungo huyo amedokeza anaweza kuanza kazi akiwa kocha.

Nguli huyo alicheza kwa kiwango bora AC Milan aking'ara katika nafasi ya kiungo mshambuliaji (namba nane) akicheza kwa mafanikio na mwaka 2008 alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia.

Klabu alizowahi kucheza Kaka ni Sao Paulo, AC Milan na Real Madrid. Kipaji chake kiling'ara zaidi akiwa Makao Makuu San Siro, Italia.