Kagere ataka Sh180mil Yanga

Mshambuliaji wa kimataifa wa Gor Mahia Meddie Kagere.

Muktasari:

  • Uongozi wa Yanga tayari umeweka wazi unataka kusajili wachezaji bora katika eneo la kipa, beki wa kati, kiungo mchezeshaji na mshambuliaji kuziba mapengo ya kipa Youthe Rostand, beki Vincent Bossou, kiungo mchezeshaji Haruna Niyonzima, Simon Msuva na mshambuliaji Donald Ngoma.

Dar es Salaam. Wakati mshambuliaji wa kimataifa wa Gor Mahia Meddie Kagere akitaka Sh180 milioni kujiunga na Yanga, klabu hiyo italazimika kutoa zaidi ya Sh500milioni ili kuboresha kikosi hicho.

Uongozi wa Yanga tayari umeweka wazi unataka kusajili wachezaji bora katika eneo la kipa, beki wa kati, kiungo mchezeshaji na mshambuliaji kuziba mapengo ya kipa Youthe Rostand, beki Vincent Bossou, kiungo mchezeshaji Haruna Niyonzima, Simon Msuva na mshambuliaji Donald Ngoma.

Kamati Maalum ya Usajili inayoongozwa na Rais wa zamani wa Yanga, Tarimba Abbas, italazimika kuvunja benki kupata saini za nyota hao akiwemo Kagere.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Rwanda, anawindwa na klabu tatu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga, Azam na Singida United ambazo kila moja inawania saini yake katika kipindi hiki cha usajili.

Akizungumza kwa simu kutoka Kenya jana, Kagere alisema klabu ya Tanzania inayomtaka iweke mezani Sh180 milioni na mshahara Sh 11 milioni kwa mwezi ndipo amwage wino.

Fedha hizo zinaweza kuwa mtihani wa kwanza kwa Kamati Maalum ambayo imepewa jukumu la kuisuka Yanga, baada ya msimu uliopita kutetereka katika michuano ya Ligi Kuu.

Kagere, aliyeibuka mfungaji bora mwaka jana na mwaka huu katika michuano ya Sport Pesa Super Cup, anatajwa kuwa ndiye mrithi halisi wa mshambuliaji Donald Ngoma aliyetua Azam. Endapo Yanga itafanikiwa kupata saini yake itakuwa imemaliza utata katika nafasi ya ushambuliaji kutokana na ubora wa Kagere katika kufunga mabao.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alisema fedha anazotaka Kagere ni nyingi kulingana na mazingira ya klabu hiyo kwa sasa.

Mkwasa alisema Yanga inasaka mshambuliaji hodari wa kigeni, lakini dau la Kagere ni kubwa na klabu hiyo haiwezi kutoa fedha hizo.

“Ni kweli tuna tatizo katika nafasi ya kipa na ushambuliaji ambayo ni lazima tuzijaze kwa kupata wachezaji hodari ambao wataisaidia Yanga kulingana na mahitaji ya timu, lakini fedha anazotaka Kagere ni nyingi hatuwezi kutoa,” alisema Mkwasa.

Mkwasa ambaye ndiye msemaji wa kamati hiyo, alisema ana matumaini makubwa vigogo walioteuliwa watafanya kazi kwa weledi na Yanga itakuwa imara.

Alisema kupitia kamati hiyo, Yanga inatarajiwa kusajili idadi kubwa ya wachezaji hasa katika eneo la ushambuliaji alilodai lilikuwa na kasoro msimu uliomalizika.

Gazeti hili limewagusia baadhi ya wachezaji ambao wanaweza kuivusha kwa kutazama bajeti ya wachezaji watatu wazawa waliong’ara katika Ligi Kuu msimu uliopita ambao wanaweza kuziba vyema mapengo katika kikosi.

Benedict Tinoco/ Aaron Kalambo

Yanga imekuwa na tatizo la kipa baada ya Youthe Rostand kucheza kwa kiwango cha chini huku namba mbili wake Beno Kakolanya akiwa nje muda mrefu kutokana na majeraha.

Tinocco amebakiza mwaka mmoja Mtibwa Sugar na thamani yake inakadiriwa kufika Sh60 milioni, wakati Kalambo pia ana mkataba na kama Yanga inataka huduma yake inatakiwa kutoa Sh25 milioni.

Juuko Murshid

Beki wa kimataifa wa Uganda amekuwa katika kiwango kizuri, lakini ameshindwa kupata namba ya kudumu katika kikosi cha Simba kutokana na sababu za nje ya uwanja, thamani ya Murshid kwa sasa ni euro 150,000 kwa mujibu wa mtandao wa www.transfermarkt.com.

Kiwango chake na uzoefu wake wa mashindano ya kimataifa unaweza kuwa msaada mkubwa kwa Yanga inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Mohammed Fakhi

Baada ya kucheza kwa kiwango bora Kagera, Fakhi amemaliza mkataba wake na klabu hiyo, lakini anaweza kuwa mbadala wa Kelvin Yondani au Andrew Vincent ‘Dante’ pindi mmojawapo anapokosekana katika kikosi hicho. Thamani ya beki huyo inaweza kufikia Sh30 milioni.

Hassani Dilunga

Ni mchezaji bora wa Kombe la Shirikisho ambaye kiwango chake kimepanda tangu alipojiunga na Mtibwa Sugar amebakiza mwaka mmoja katika mkataba Yanga inaweza kumrejesha kiungo wake huyo wa zamani kwa Sh40 milioni.

Bigirimana Blaise

Mshambuliaji Mrundi amekuwa katika kiwango bora katika kikosi cha Stand United msimu huu amefunga mabao matatu na sasa ameanza kuwaniwa na KMC hiyo ni ishara thamani yake haitozidi Sh30 milioni.