Enrique aibuka tena Arsenal

Friday April 13 2018

 

LONDONENGLAND

ALIYEKUWA Kocha wa Barcelona, Luis Enrique ameibuka tena kwenye mipango ya kwenda kuwa kocha wa Arsenal kwa kuchukua mikoba ya Arsene Wenger.

Ripoti za kutoka Hispania zinadai mabosi wa Arsenal wameamua kuanzisha upya mazungumzo na wawakilishi wa kocha huyo kwa ajili ya kumpa kibarua cha kwenda kuinoa timu hiyo yenye maskani yake huko Emirates.

Enrique amekuwa akihusishwa pia na Chelsea, lakini wababe hao wa Stamford Bridge kwa sasa wameonekana kuwa na mpango mbadala wakitaka kuajiri kocha mwingine kabisa au kuendelea kubaki na Antonio Conte.

Arsenal sasa imekoleza moto wake wa kumfukuzia ikiamini ndiye mtu mwafaka wa kumrithi Mfaransa Wenger ambaye ameonekana kutokuwa na maajabu kwenye kikosi hicho kwa miaka ya karibuni baada ya kumaliza mwaka wa 14 sasa bila ya taji la Ligi Kuu England, kitu ambacho ndio hamu kubwa ya mashabiki wa timu hiyo.