England yamaliza ‘uteja’ wa vipigo

Muktasari:

  • Ushindi katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa King Power wa timu ya Leicester City, umemwezesha Kocha wa England, Gareth Southgate kupumua baada ya kujiondoa kwenye kipindi kigumu cha matokeo ya kuumiza.

Leicester, England. Hatimaye timu ya Taifa ya England, imemaliza jinamizi lililoiandama la vipigo vitatu  mfululizo baada ya jana Marcus Rashford kuifungia bao pekee ilipoilaza Uswisi 1-0, katika mechi ya kirafiki ya kimataifa.

Ushindi katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa King Power wa timu ya Leicester City, umemwezesha Kocha wa England, Gareth Southgate kupumua baada ya kujiondoa kwenye kipindi kigumu cha matokeo ya kuumiza.

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 20 England ilijikuta ikipoteza mechi tatu mfululizo baada ya kufungwa na Croatia mabao 2-1 katika nusu fainali ya Kombe la Dunia na baadaye kufungwa na Ubelgiji 2-0 katika mechi ya kusaka nafasi ya tatu kabla ya kufungwa 1-0 na Hispania katika mechi ya mashindano ya ‘Euro Nations League’.   

Mshambuliaji chipukizi asiye na uhakika wa namba katika timu yake ya Manchester United, Marcus Rashford ndiye aliyeifungia nchi yake bao hilo muhimu katika dakika ya 54 akiunganisha krosi ya mlinzi Kyle Walker.

Kocha Southgate atafurahia uamuzi wake wa kutumia washambuliaji wawili mbele ambapo Rashford alishirikiana na Danny Welbeck huku nyuma yao kukiwa na viungo watano jambo lililomaanisha kuwa walipania kucheza kwa kujilinda licha ya kuwa nyumbani.

Kiungo nyota wa Uswisi, Xherdan Shaqiri alikaribia kuwafunga wenyeji mara mbili katika kipindi cha kwanza ambapo shuti lake la hatari zaidi liligonga mwamba kabla ya kuokolewa.