Dar yazoa dhahabu Coca Cola Umisseta

Wednesday June 13 2018

 

By Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz

Mwanza. Joto la mashindano ya Copa Coca Cola Umisseta limepanda huku timu za wavu, netiboli, soka, kikapu na riadha za mkoa wa Dar es Salaam zikitawala katika mechi zinazochezwa viwanja vya Chuo cha Ualimu Butimba.

Dar es Salaam imetinga nusu fainali kwenye mchezo wa wavu, mpira wa kikapu, netiboli, soka na imeshinda medali za dhahabu kwenye riadha katika mbio za mita 100 kwa wavulana, wasichana na medali ya fedha ya ‘relay’ mita 400 wavulana.

Wanariadha, Ismail Tosi aliyekimbia kwa sekunde 11:31 na Winfrida Makenji aliyetumia sekunde 12:50 waliipa Dar es Salaam medali za dhahabu za mbio fupi mita 100 katika mashindano hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Coca Cola Tanzania.

“Nilijiandaa kushinda, nimekuwa nikijifua kwa juhudi na bidii ili nifanye vizuri, ndoto niliyonayo ni kuwa mwanariadha wa kimataifa,” alisema Makenji.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na Basra Abdallah wa Unguja aliyekimbia kwa sekunde 12:86 na Rehema John wa Mwanza alihitimisha tatu bora akikimbia kwa sekunde 12:94.

Upande wa wavulana, Mohammed Amour aliyekimbia kwa sekunde 11:54 na Omari Said sekunde 11:62 wote wa Unguja walitwaa medali ya pili na tatu.

Kwenye mpira wa wavu, Dar es Salaam wasichana ilifuzu nusu fainali ya michuano hiyo kwa kuichapa Katavi seti 3-0 za pointi 25-15, 25-3 na 25-19.

Katika mpira wa kikapu, Dar es Salaam tena iliisurubu Mtwara kwa kuichapa vikapu 103-15 katika robo fainali ya kwanza.

Kwenye netiboli, Dar es Salaam pia imepenya katika nusu fainali na inapewa nafasi ya kucheza fainali dhidi ya Morogoro ambayo imeingia baada ya kuichapa Singida mabao 64-19.