Chelsea kuchagua moja Hazard au Conte

Tuesday May 15 2018

 

LONDON, ENGLAND

CHELSEA sasa ina shughuli moja ya kuchagua kusuka au kunyoa juu ya watu wake wawili, Eden Hazard na Antonio Conte.

Supastaa wa timu hiyo, Hazard amefichua yupo tayari kuihama Chelsea kama Conte ataendelea kuwa kocha wa timu hiyo msimu ujao.

Kumekuwa na taarifa kuwa uhusiano wa Conte na Hazard umekuwa mbovu kwa msimu huu na jambo hilo linawafanya wawili hao wasiwe na uhakika wa kufanya kazi nzuri wakiendelea kuwa pamoja Stamford Bridge.

Hazard amegoma kusaini mkataba mpya katika klabu hiyo akisubiri kuona mwenendo wa klabu utakavyokuwa baada ya kumaliza msimu nje ya Top Four na hivyo kukosa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Chelsea sasa inafikiria kuajiri kocha mpya huku ikipiga hesabu za kuwanasa Luis Enrique na Maurizio Sarri na inamini hilo likifanyika basi itaweza kumshawishi winga huyo wa Kibelgiji kuendelea kubaki kwenye kikosi chake.

Ripoti zinadai Conte amegoma kuachia ngazi akisubiri Chelsea imfukuze kwa sababu jambo hilo litamfanya kulipwa Pauni 9 milioni za fidia na Chelsea ipo tayari kulipa mkwanja huo kama Hazard atakubali kusajili dili jipya lenye thamani ya Pauni 300,000 kwa wiki kubaki klabuni hapo.