Boko waihemsha Victoria Group

Muktasari:

  • Mchezo huo maalumu ulilenga kumuenzi Baba wa Taifa ambaye alikuwa mpenda michezo pamoja na kuimarisha afya.

Timu ya Boko Veterans jana iliwatambia Victoria Group kwa kuichapa mabao 5-2, katika mchezo maalumu, uliokuwa na lengo la kumuenzi, hayati Mwalimu Baba wa Taifa, Julius Nyerere.

Mchezo huo ambao ulichezwa katika Uwanja wa Boko Veterans, Boko jijini Dar es Salaam na ulihudhuriwa na watu 'wazito' kutoka kampuni mbalimbali nchini.

Kikosi cha Boko Veterans kilikuwa na wachezaji wakali kama, Emmanuel Kanagisa 'Adebayor',  Athuman Tippo wa Zizou fation, wakati Victoria Group kiliundwa na wachezaji kama, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications LTD (MCL) , Francis Nanai na Mjumbe wa Bodi hiyo, John Ulanga.

Akizungumzia mchezo huo, Ngeleja alisema: "Lengo ni kumuenzi hayati Baba wa Taifa ambaye alikuwa ni mpenda michezo, kuimarisha afya zetu katika michezo pamoja na jamii nzima lakini pia na kuendeleza umoja wetu."

Katika bonanza hilo, Kampuni ya Mwananchi Communications LTD kupitia gazeti la Mwanaspoti, ilikuwa sehemu ya wadhamini.