Griezmann: ‘Bishoo’ anayesumbua Ulaya

Muktasari:

Griezmann alitua Atletico kuchukua mikoba ya straika wake matata, Diego Costa, ambaye alikuwa ametoka kuipa taji la La Liga kisha akatimkia zake Chelsea.

MWAKA 2014, Atlético Madrid ililipa dau la Euro 30 milioni kwa klabu ya Real Sociedad kwa ajili ya kupata huduma ya Antoine Griezmann.

Griezmann alitua Atletico kuchukua mikoba ya straika wake matata, Diego Costa, ambaye alikuwa ametoka kuipa taji la La Liga kisha akatimkia zake Chelsea.

Uhamisho wa staa huyo wa Kifaransa uliwashangaza wengi kwani, hakuwa akifahamika sana kwenye soka la ushindani barani Ulaya.

Lakini, Griezmann aliyezaliwa Machi 21, 1991 mjini Macon, Ufaransa hakuonekana kuwa na hofu, ambapo kwenye mechi zake za awali tu alianza kuonyesha kuwa anastahili kuwepo kwenye kikosi hicho.

Tangu alipotua kwenye kikosi cha Atletico, kiwango cha Griezmann kilianza kutikisa soka la Ulaya na kuwa mchezaji tegemeo huku akipasia nyavuni na kutengeneza asisti kibao za mabao. Jina lake likazidi kupaa na hapo ndipo klabu kubwa zikaanza kumfuatilia, lakini nyota yake ilikuja kung’ara zaidi kwenye michuano ya Euro 2016 kule Ufaransa.

Griezmann alikiongoza vyema kikosi cha Didier Deschamp kufika fainali, ambapo walipoteza kwa Ureno kwenye fainali ambayo ilitawaliwa na ufundi mwingi.

Ni fainali hizo ndio zilimweka kwenye matawi ya juu, ambapo aliibuka kuwa Mfungaji Bora wa michuano hiyo na kwa mara ya kwanza akatajwa kwenye orodha ya kuwania tuzo za Ballon d’Or 2016.

Hata hivyo, hakuweza kufurukuta mbele ya Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, ambapo alishika nafasi ya tatu huku tuzo hiyo ikienda kwa Ronaldo ambaye aliipa Ureno taji hilo kwa mara ya kwanza.

Baada ya hapo jina lake likakamata kwenyea anga za usajili, ambapo Manchester United walitangaza kutaka huduma yake akitajwa kuwa mrithi sahihi wa Wayne Rooney na Zlatan Ibrahimovich.

Hata hivyo, Griezmann walifikia makubaliano binafsi na Man United, lakini dili hilo lilikwama kutokana Atletico kufungiwa kusajili na staa huyo mwezi Juni akasaini mkataba mpya kuendelea kuwepo klabuni hapo.Hata hivyo, Man United, Barcelona na Real Madrid zimeibuka kukabana koo kuwania huduma ya staa huyo kwenye dirisha la usajili la Januari, mwakani. Kwa sasa tu anapiga pesa za maana na kama akiamua kuondoka na kutua Man United, Barca au Real Madrid basi atavuna mkwanja wa mrefu na kuingia mikataba minono na kampuni binafsi kama ilivyo kwa mastaa wengine duniani.

Anamiliki mijengo ya maana na magari ya kifahari huku akiwekeza fedha zake kwenye miradi mbalimbali mikubwa na kuifanya familia yake kuishi maisha bora.