Beki tatu unaotamani wahamie timu yako

Muktasari:

  • Lakini, kwa soka la kisasa, mambo ya mabadilika sana, mabeki wa kushoto au wa pembeni kwa ujumla wamekuwa wakitarajiwa kufanya mambo makubwa zaidi ya kukaba. Mabeki wa pembeni wa sasa ni ngumu kuwatofautisha na mawinga kwa kile wanachokifanya kwenye mechi, kwa sababu muda wote wapo kwenye eneo la penalti la timu pinzani, kupandisha mashambulizi, lakini shughuli yao ya kukaba pia wakiifanya kwa usahihi.

LONDON, ENGLAND

MIAKA 20 iliyopita, kazi ya mabeki wa kushoto ilikuwa kukaba tu na mengine machache sana. Lakini, kwa soka la kisasa, mambo ya mabadilika sana, mabeki wa kushoto au wa pembeni kwa ujumla wamekuwa wakitarajiwa kufanya mambo makubwa zaidi ya kukaba. Mabeki wa pembeni wa sasa ni ngumu kuwatofautisha na mawinga kwa kile wanachokifanya kwenye mechi, kwa sababu muda wote wapo kwenye eneo la penalti la timu pinzani, kupandisha mashambulizi, lakini shughuli yao ya kukaba pia wakiifanya kwa usahihi.

Hawa hapa mabeki wa kushoto matata kabisa mabao kila shabiki wa soka angependa kumwona anacheza kwenye timu yake.

5.Alex Sandro (Juventus)

Huyu ni beki wa kushoto ambaye hapewi sana sifa, lakini shughuli yake ya ndani ya uwanja si mchezo. Kwenye soka la kimataifa, Sandro amekuwa akitambukwa pia, kwa sababu nafasi anayocheza kuna mtu mwingine balaa zaidi, anaitwa Marcelo. Hilo ndilo tatizo linalomkabili Sandro, kwamba amekuja kwenye wakati mbaya, kuna Marcelo. Lakini, zaidi ya hapo ni beki wa pembeni mwenye uwezo mkubwa wa kukaba na kushambulia. Ukiwa naye kwenye kikosi, huhitaji winga.

4.Marcos Alonso (Chelsea)

Ni mara chache sana kupata beki wa kushoto mwenye uwezo wa kupanda na kushuka kwa kasi ileile na mara zote anakuwa kwenye eneo la penalti la timu pinzani.

Utashangaa staa huyo wa Chelsea amehusika kwenye asisti nyingi, wakati yeye ni beki, lakini kubwa linalofanya hivyo ni uchezaji wake, kwamba muda wote yupo kwenye eneo la wapinzani licha ya kuyatimiza pia vyema kabisa majukumu yake ya kukaba.

Marcos Alonso amepewa kazi pia ya kupiga mipira yote ya friikiki huko kwenye kikosi cha Chelsea.

3.Benjamin Mendy (Man City)

Si mtu aliyekuwa akifahamika sana na mashabiki wa soka huko nyuma, lakini kwa sasa wengi wao wanamfahamu Benjamin Mendy ni nani.

Kama ilivyo kwa mabeki wengine wa kushoto, Mendy naye amekuwa moto kweli kweli katika kushambulia, huku akitimiza pia majukumu yake ya msingi katika kuzuia mashambulizi.

Mendy anapokuwa nyuma ni beki, lakini anapokwenda mbele na mpira anakuwa mshambuliaji na kuleta madhara makubwa kwa timu pinzani. Manchester City ililipa pesa nyingi kupata huduma yake.

2.David Alaba (Bayern Munich)

Kwenye timu yake ya taifa, David Alaba anacheza nafasi ya kiungo wa kati na hii ni kwa sababu amekuwa mpigaji wa pasi mahiri sana.

Lakini, staa huyo wa kimataifa wa Austria, yeye nafasi yake ya asili ni beki wa kushoto. Hakika miguu yake ina ujuzi mkubwa wa kuuchezea mpira na ndio maana panga pangua amekuwa hakosi kwenye kikosi cha Bayern Munich.

Alaba amekuwa akitengeneza kombinesheni nzuri na mawinga wa Bayern, hususani Franck Ribery na hakika wapinzani wamekuwa wakipata tabu sana.

1.Marcelo

(Real Madrid)

Kwa muda mrefu sasa, Marcelo amekuwa beki wa kushoto bora kabisa duniani. Hakuna shabiki wa soka ambaye asingependa kuwa na huduma ya Mbrazili huyo kwenye kikosi chake.

Ni jambo la wazi, anapokosekana kwenye kikosi cha Real Madrid pengo lake linaonekana wazi kwa sababu kikosi hicho kinakuwa hakina makali yake ya asili kwenye safu ya ushambuliaji.

Marcelo anapopanda mbele kushambulia, anakuwa mchezaji tofauti kabisa, huwezi kumdhania kuwa ni beki, kwa sababu ya utulivu aliokuwa nao, asipofunga mwenyewe basi anapiga pasi ambayo kwa aliyepigiwa akishindwa kufunga basi hilo ni tatizo lake binafsi. Hakika Real Madrid na Brazil zimepata mrithi sahihi wa Roberto Carlos.